Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar (hawapo pichani) walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma Wajumbe wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar wakimsikiliza Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga (hayupo pichani), walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.
Picha na RFB
************************
Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyauhenga, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa kwenye miundombinu ya barabara hapa nchini kwa kuongeza fedha za kugharamia ujenzi na matengenezo ya barabara.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na ujumbe kutoka Mfuko wa Barabara Zanzibar uliomtembelea ofisini kwake mtaa wa Ammar, Jijini Dodoma.
“Kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitenga zaidi ya Shilingi bilioni 440 kila mwaka mahsusi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara za mijini na vijijini. Hatua hii imepelekea kuimarika kwa kiwango kikubwa kwa mtandao wa barabara za vijijini. Hii ni pamoja na kufungua barabara nyingi ambazo zilikuwa hazipitiki hapo awali. Maboresha haya yanawawezesha wananchi kufikia na kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi zinazopatikana kutokana na miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ” amesema Nyauhenga.
Nyauhenga, ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (Kanda ya Afrika Mashariki), ameuambia ujumbe huo kuwa makusanyo ya fedha za kugharamia matengenezo ya barabara yameongezeka kwa asilimia 27 kutoka Shilingi bilioni 806.7 mwaka wa fedha 2019/20 hadi Shilingi bilioni 1,027 mwaka wa fedha 2021/22. Aidha, kwa miaka yote mitatu iliyopita, Serikali imekuwa ikitoa fedha zote za kugharamia matengenezo ya barabara kama zinavyoidhinishwa na Bunge. Hatua hii imewezesha kutekeleza kazi nyingi za matengenezo ya barabara na hivyo kulinda thamani ya uwekezaji wa Serikali kwenye miundombinu yake na kuwawezesha watumiaji wengi wa barabara kupata huduma nzuri za usafiri na usafirishaji.
Ameongeza kuwa Serikali ilianzisha Mfuko wa Barabara Tanzania mwaka 2000 kupitia Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220 ili kugharamia kikamilifu matengenezo ya barabara zote za Tanzania Bara. Chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko huo ni tozo za mafuta, kiasi cha shilingi 363 kwa kila lita ya dizeli na petrol. Alitaja vyanzo vingine kuwa ni tozo kwa magari ya kigeni yanayotumia barabara nchini pamoja na faini zinazotozwa kutokana na uzidishaji uzito wa magari.
Nyauhenga amechukua fursa hiyo kuwaasa wananchi kutunza miundombinu ya barabara kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuzilinda samani za barabara, kutupa takataka kwenye mifereji ya barabara, kutokutiririsha maji na kutopitisha mifugo barabarani. Hii ni kwa sababu Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara na pia ndiyo njia ya usafiri na usafirishaji inayotumiwa zaidi hapa nchini. Hivyo uharibifu wake huleta hasara kubwa kwa Serikali na kuwafanya wanachi wengi kukosa huduma za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar, CPA Bakari Rashid, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunda Kamati hiyo ili kuboresha matumizi ya barabara za Zanzibar na kwamba Kamati yake tayari imetembelea barabara zote za Unguja na Pemba kabla ya kuamua kutembelea Mfuko wa Barabara Tanzania Bara.
Naye Omar Makame ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar, amemshukuru Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania kwa kukutana nao kuwa Kamati zao zimejifunza mambo mengi kuhusu uendeshaji wa Mfuko wa Barabara na kwamba Mfuko wa Barabara Zanzibar utaendeleza ushirikiano madhubuti uliopo baina ya Mifuko hii miwili nchini.
Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar pamoja na Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar zipo mkoani Dodoma kwa ziara ya siku mbili, ili kujifunza na kujionea utendaji kazi wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara.