Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 5.2 kwa hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ili kuboresha huduma za afya za akina mama wanaojifungua katika hospitali hiyo.
Msaada huo unaolenga kugharamua ununuzi wa mashine za kisasa za kupima presha ( Digital BP Machines) sita, viti mwendo ( wheel chairs) viwili, vitanda vya uchunguzi ( examination beds) vinne na vifaa vya kujifungulia ( delivery kits) kumi( 10) umekabidhiwa kwa Mganga Mkuu wa jiji la Mwanza, Dkt Pima Sebastian na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa EWURA kinachofanyika jijini Mwanza.
“ EWURA mmetutoa kimasomaso, kwa kweli mmeshirikiana nasi kwenye mambo mengi katika mkoa wetu wa Mwanza, ujenzi wa madarasa, ujenzi wa ofisi na sasa kuokoa maisha ya watanzania wenzetu, tunawashukuru sana, tunaomba muendelee na moyo huo, na nitoe mwito msaada huu uwe chachu ya kuboresha huduma zetu”. Alisema Mhe.Makilagi
Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA, Mha. Poline Msuya, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA na Mwenyekiti wa Baraza, Dkt James Andilile, alieleza kuwa, EWURA imekua na utaratibu wa kutoa misaada kwa kadiri inavyowezekana katika nyanja mbalimbali kwenye jamii ikiwamo afya, elimu, majanga na maeneo mangine kadha wa kadha ili kuonesha athari ya udhibiti kwenye kuimarisha huduma mbalimbali zinazoigusa jamii moja kwa moja.
“ Sisi EWURA, tunamuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma mbalimbali ikiwamo afya, hivyo tumeona kwa kipindi hiki tushirikiane na wenzetu wa Mwanza katika kutatua changamoto kiasi kwenye hospitali ya Nyamagana”. Alieleza Mha. Msuya
Alizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi ya msaada huo, Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Dkt Pima Sebastian ameahidi kuwa, atahakikisha vifaa tiba vitakavyonunuliwa,vinatumika kwa lengo lililokusudiwa.
“Ninatoa pongezi kwa utendaji uliotukukau wa EWURA, na ninatoa shukrani za dhati kwa msaada huu, ambao utatusaidia kwa kiasi kikubwa, ninaahidi malengo kusudiwa yatatekelezwa”. Alieleza Dkt Sebastian
Aidha, Mganga Mkuu huyo alieleza kwamba, wanawake takribani 600 hujifungua katika hospitali ya Nyamagana kwa mwezi, na kwamba hospitali hiyo hutoa huduma ya kliniki kwa mama wajawazito kati ya 3500-4500 kwa kipindi hicho, hivyo uhitaji wa vifaa tiba bado ni mkubwa.