Afisa Uhusiano wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Dorine Denis (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madarasa mawili yaliyojengwa na kampuni hiyo katika Shule ya Msingi Kiziba iliyopo Kijiji cha Mwenegeza wilayani Geita. Dorine alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong. Kushoto ni Mtendaji wa Kata ya Nyakagomba, Christopha Amos.
Na Mwandishi Wetu - Geita
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu na kulea kizazi kijacho ambacho kitasaidia Taifa kufikia malengo ya kiuchumi na kimaendeleo, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imejenga na kukabidhi vyumba viwili vya madarasa kwa Shule ya Msingi Kiziba iliyopo Kijiji cha Mwenegeza kata ya Nyakagomba, Wilayani Geita mkoani Geita.
Madarasa hayo mawili yenye thamani ya Sh milioni 42, yanalenga kusaidia kutoa mazingira mazuri ya kujifunzia kwa wanafunzi ambao ufaulu wao umeathiriwa na mazingira magumu ya kujifunza.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi madarasa hayo mwishoni mwa wiki mjini Geita kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong, Afisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Dorine Denis alisema elimu ni nguzo muhimu ya jamii hivyo bila elimu,ni vigumu kupata maendeleo.
Alisema elimu inaweza kubadilisha maisha ya watu na ni mwelekeo wa miradi yetu ya uwekezaji wa jamii.
“GGML inaamini kuwa wananchi wa Tanzania ndio mtaji mkubwa wa kampuni hii na siku zote imekuwa ikiunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu na kujenga kizazi kijacho ambacho kitasaidia taifa la Tanzania kufikia malengo yake makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.
“GGML imedhamiria kuchochea maendeleo endelevu ya jamii zinazozunguka mgodi na imedhihirisha hilo mara kwa mara kwa kushirikiana kikamilifu na serikali katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na barabara pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka mgodi huo.
“Tunakusudia kuwa na urithi uliojengwa na uchumi endelevu wa ndani unaoweza kukaa muda mrefu hata baada ya shughuli za uchimbaji madini mkoani Geita kumalizika,” alisema.
Alisema GGML inafanya kazi ya kuunga mkono malengo ya serikali ya Tanzania ya ukuaji thabiti wa uchumi na maboresho ya miundombinu ya kijamii.
“Hii inaendana na thamani yetu ya msingi ya kusaidia serikali katika kukuza ukuaji wa uchumi wa muda mrefu katika jamii tunakofanyia kazi. Kwa hiyo nimefurahishwa kwamba ujenzi wa madarasa haya umetokana na juhudi za ushirikiano kati ya serikali, jamii mwenyeji na GGML,” alisema.
Aidha, aliahidi kuwa GGML itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania na wadau wengine ili kufikia lengo la sekta ya madini la kuchangia asilimia 10 katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.
Naye Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kiziba Beatus Mwandu aliishukuru GGML kwa ujenzi wa madarasa hayo hasa ikizingatiwa shule hiyo bado inakabiliwa na uhaba wa madarasa huku mengine yakiwa yamechakaa.
Aidha, Mtendaji wa Kata ya Nyakagomba, Christopha Amos naye aliishukuru GGML kwa msaada huo na kuahidi pia kufikisha kilio cha changamoto nyingine kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili azifanyie kazi.