*******************************************
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo; Imam Khomeini (M.A) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alirejea nchini Iran na kulakiwa na umati mkubwa wa wananchi, baada ya kuwa uhamishoni kwa zaidi ya miaka 10; siku ambayo imebakia kuwa moja ya siku za kihistoria zenye kukumbukwa mno katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Kwa hakika Tarehe 12 Bahman 1357 iliyosadifiana na Februari Mosi, 1979 Miladia, ilikuwa nukta kuu katika mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah; na katika kipindi cha siku kumi tu tangu kurejea nchini Imam Khomeini, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi licha ya uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Shah.
Baada ya Mfalme Shah kibaraka wa madola ya Magharibi kukimbia nchi hapo tarehe 26 Dei 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 16 Januari 1979, Imam Khomeini alitangaza uamuzi wake wa kurejea nchini.
Uamuzi huo wa kishujaa na wa hatari pia uliwatia wasi wasi mkubwa wapenzi na wapinzani wa mtukufu huyo.
Wananchi wa Iran na licha ya kwamba walikuwa wamefanya subira ya muda mrefu ya kumgonjea kiongozi wao huyo, pia walikuwa na wasi wasi kwamba vibaraka wa utawala wa kitwaghuti watamsababishia madhara katika safari yake hiyo ya kurejea nchini.
Kwa upande mwingine nao utawala wa Shah na waungaji mkono wake wa Kimarekani na Wamagharibi walikuwa wanajua kwamba, kurejea Imam Khomeini nchini Iran kutazidisha moto wa harakati za kimapinduzi na hatimaye kufikiwa ushindi wa Mapinduzi hayo ya Kiislamu.
Baada ya Imam kuazimia kurejea nchini, kulianza harakati nyingi za kuzuia safari yake hiyo ya kihistoria.
Mkabala wake wanamapinduzi miongoni mwa wananchi walitumia uwezo wao wote kwa ajili ya kuzishinda njama hizo za maadui ili kufanikisha kiongozi wao huyo anawasili nchini salama salimini.
Wananchi walioshikamana na dini wa Iran walikuwa pamoja na Imam Khomeini baada ya kuitikia mwito wake wa kuchukia dhulma.
Wananchi wa Iran walikuwa wameona kuwa, Imam Khomeini alikuwa mtu safi, arif na aliyekuwa akiguswa mno na mambo ya wananchi na hakuwa akifanya hayo kwa ajili ya hawaa na matamanio bali alikuwa kama Imam Hussein AS ambaye alitoka na kuanzisha harakati kwa ajili ya kuhuisha dini na thamani za Uislamu.
Ni kwa msingi huo ndio maana wananchi wa Iran wakaitikia mwito wake, na kusimama naye bega kwa bega kukabiliana na dhulma na ukndamizaji wa utawala wa mfalme Shah.
Imam Khomeini kama walivyokuwa mababu zake watoharifu, alikuwa katika harakati na mkondo wa kulea watu na jamii na katika sentesi moja tunaweza kusema kuwa, alikuwa akifuatilia suala la kueneza maadili mema.
Kueneza maadili na tabia njema ni miongoni mwa amri za Mwenyezi Mungu katika Qur’ani kwa Nabii wake Mtukufu Muhammad SAW, ili wale wote wanaotaka kuingia katika Uislamu wafahamu kwamba, utawala na siasa sio mambo ambayo yako kando na utukufu wa mwanadamu na masuala ya kimaanawi; bali jamii bora ya Kiislamu itafikia daraja hiyo kwa kufungamana tu na masuala haya mawili muhimu.
Mwenyezi Mungu SWT anawakumbusha Waislamu kuhusiana na hili katika Aya ya 21 ya Surat al-Ah’za kwa kusema:Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.
Kwa hakika Mtume SAW alikuwa ruwaza njema ya juu kabisa ya mtawala wa Kiislamu na baada yake, Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye alichoroa na kudhihirisha umbo la uadilifu wa kijamii na utukufu wa mwanadamu katika kipindi cha utawala wake wa Kiislamu.
Imam Khomeni pia akifuata nyayo za shakhsia wakubwa wa kidini, alikuwa katika mkondo wa kuhuisha na kueneza thamani za kidini katika jamii.
Jamii ambayo itajengwa katika misingi ya Uislamu na fikihi ya Kishia na hivyo, tabia njema, maadili mema, bila shaka masuala ya kimaanawi hujitokeza na kudhihirika bayana katika jamii hiyo.
Hapana shaka kuwa, utawala kama huu ulikuwa ukihitajia kiongozi ambaye yeye mwenyewe amebobea katika taaluma ya fikihi, mwenye utambuzi sahihi na mpana wa dini, aliyejipamba kwa taqwa na uchaji Mungu na maadili mema; ambapo Imam Khomeini alikuwa na sifa zote hizi.
Mwanzoni mwa ujana wake, Imam Khomeini alijishuhulisha na kulea nafsi yake na kujibidiisha katika kujiimarisha zaidi katika maadili mema na sifa njema.
Kwa hakika shakhsia huyo hakuwa na mithili katika kuchunga maadili na kushikamana na taqwa na kumuogopa Mwenyezi Mungu.
Walioishi chumba kimoja na Imam Khomeini wakati akiwa masomoni walikuwa wakifahamu kwamba, Ruhullah Khomeini ana sifa kuu mbili: Sifa ya kwanza ni kuamka usiku wa manane kwa ajili ya kuswali Swala ya Suna ya usiku.
Sifa ya pili ni kujiweka mbali kabisa na kusengenya watu, bali hata kusikiliza watu wakisengenya.
Shakhsia wa namna hii alikuwa akitilia mkazo mno suala la kusema kweli na kutenda mema, na inawezekana kusema kuwa, ‘ukweli katika kauli na matendo’ ni vigezo ambavyo viliwavutia zaidi watu katika shaksia ya Imam Khomeini (Rahmatullah Aleih)Kusema kweli tupu na kujiepusha na uongo ni katika maamrisho ya Mwenyezi katika Qur’ani pamoja na miongozo ya viongozi wa dini na wakati huo huo ni miongoni mwa ishara za imani, taqwa na uchaji Mungu.
Imam Ali AS anasema: Kusema kweli ni nguzo imara kabisa ya dini.
Imam Khomeini alikuwa mtiifu kwa kile alichokuwa akikisema iwe ni katika maisha yake binafsi au maisha yake ya kisiasa.
Alipokuwa akiwanasihi maafisa wa serikali na suala la kutoikumbatia dunia na kuishi maisha ya kawaida yasiyo na ufakhari, basi yeye alikuwa kigezo cha kweli kabisa katika hayo.
Wakati wananchi wa Iran walipoona tamu ya ukweli katika maneno na vitendo vya Imam Khomeini (Quddisa Sirruh) walimuamini na kuwa pamoja naye zaidi katika njia yake ya Mapinduzi na ni katika mazingira haya ndipo wananchi Waislamu wa Iran wakawa tayari kufa shahidi katika njia ya kumtetea na kumhami kiongozi wao huyu.
Imam Khomeini alikuwa Marjaa mkubwa wa kidini na arif na wakati huo huo mwanasiasa mahiri, mwenye upeo wa hali ya juu, aliyekuwa na shakhsia ya kuvutia na yenye ushawishi kwa watu, aliyekuwa dhidi ya udikteta na ambaye hakuwa na utegemezi siyo kwa madola makubwa ya Magharibi wala ya Mashariki.
Kwa upande wa busuri na muono wa mbali sambamba na mtazamo wa kina kuhusiana na masuala ya jamii alikuwa na upeo na ustadi wa aina yake katika zama zake, kama ambavyo alikuwa mweledi wa masuala ya mataifa mengine ya dunia.
Aidha Imam Khomeini alifahamika kwa kuwa mtu wa ratiba, mipango, unadhifu na utanashati, na moja ya siri za mafanikio yake ni kwamba, alikuwa na mipango madhubuti ya kielimu na kivitendo, katika uongozi na hata katika harakati zake za kisiasa.
Historia inaonyesha kuwa, alikuwa akiandaa jedwali na ratiba kwa ajili ya kazi anazopaswa kufanya mathalani kesho.
Aidha jedwali hilo lilikuwa limejaa kazi na shughuli katika masaa yote isipokuwa nyakati za usiku ambapo alikuwa akiamka na kuswai Swala ya usiku na kunong’ona na Mola wake.
Imam Khomeini alikuwa na mipango maalumu na makini kiasi kwamba, watu waliokuwa wakimzunguka kwa kumuona Imam Khomeini akifanya jambo fulani basi waliweza kujua hivi sasa ni saa ngapi.
Hii ni kutokana na kuwa, Imam Ruhullah Khomeini alikuwa na wakati maalumu wa kula chakula, alikuwa na wakati maalumu wa kulala na alikuwa akiamka katika saa na wakati maalumu.
Hata anapokuwa na miadi na mtu alikuwa akifika kwa wakati bila kuchelewa hata kidogo.Sayyida Zahra Mustafavi, binti wa Imam Khomeini anasimulia kwa kusema: Imam alikuwa makini na mtu wa wakati kiasi kwamba, ikitokea amechelewa dakika chache tu kwa ajili ya chakula, watu wake wa nyumbani walikuwa wakiingiwa na wasiwasi.
Hivyo wote bila ya kupenda hujipata wameelekea katika chumba ya Imam, na wanapofika huko humkuta kwa mfano Ahmad mtoto wa Imam amewasili hapo na alikuwa akimuuliza maswali baba yake, ambaye naye hakuwa na budi isipokuwa kumjibu na hivyo kumfanya achelewe.
Tunakamilisha Makala yetu yaliyojiri kwa manasaba wa siku hizi za kumbukumbu ya Alfajiri Kumi kuelekea kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa kunukuu maneno ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa Imam Khomeini.
Ayatullah Khamenei anasema: Imam Khomeini alikuwa katika rehema na fadhila za Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa kwake na mahusiano na mafungano na Mwenyezi Mungu.
Hebu, njooni na sisi tuendeleze njia yake kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwa na ikhlasi na nia njema (katika amali na matendo yetu) na kufanya hima, idili na kuwa na azma na msimamo thabiti.
Aliyekutayarishia na kukuletea Makala hii ni mimi Salum Bendera. Nakutakieni kila la kheri. Kwaherini
####MWISHO###
Social Plugin