Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHENGERWA, DKT. ABBASI WASHIRIKI MCHEZO WA SSC NA RAJA.


*************

*Mchengerwa asisitiza kutumia Utalii wa Michezo kuitangaza Tanzania.

Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi leo ni miongoni mwa viongozi na wadau wa Soka ambao wameshiriki kwenye mpambano baina ya Simba SC na Raja CA katika mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika katika kundi C.

Mchezo huu umechezwa katika Uwanja wa Mkapa ambapo hadi mwisho wa mchezo Raja imeongoza kwa mabao matatu kwa nunge

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan alitangaza kutoa shilingi milioni tano kwa kila goli litakalofungwa na timu ya Simba leo ambapo pia atatoa fedha hiyo hiyo kesho kwa timu ya Yanga endapo itaifunga timu ya TP Mazembe katika Kombe la Shirikisho.

Mhe. Mchengerwa alikuwa waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Dkt. Abbasi alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo hadi Februari 14, 2023 ambapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliwateua tena kuendelea kuhudumu kwa nafasi hizo hizo kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa Wizara yake imedhamiria pamoja na mikakati mingine kutangaza utalii ikiwa ni pamoja na Utalii wa Michezo na Utamaduni ili uweze kuchangia kwenye pato la Taifa.

Aidha, akiongea na Menejimenti ya Wizara yake jana, Mhe. Mchengerwa amesisitiza sekta ya Utalii inatakiwa kuchangia kiasi kikubwa kwenye uchumi na pato la Taifa kwa kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na ambavyo havipatikani katika sehemu mbalimbali duniani.

Naye Dkt. Abbasi ameongeza kuwa tayari Mhe. Rais Samia Suluhu ameshafanya kazi kubwa ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia Filamu ya Royal Tour hivyo watanzania wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo.

Hadi sasa katika kundi Hilo timu ya Raja, inaongoza ikifuatiwa na Horoya, Vipers na Simba inashika nafasi ya mwisho.

Mchezo huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe Pindi Chana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com