👉Asisitiza urejeshwaji wa Mafuvu, aishukuru China.
Na John Mapepele.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kujenga makumbusho ya kisasa ambayo itakuwa kivutio kikubwa cha Utalii kitakachosaidia kuliingizia Taifa mapato na kujenga uchumi wa nchi yetu.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 20, 2023 baada ya kufanya ziara yake ya kwanza katika Ofisi za Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam akiambatana na Naibu Waziri Mhe, Mary Masanja na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi.
Mhe. Mchengerwa amesema kuna baadhi ya mataifa duniani ambayo yamefanya uwekezaji wa kutoka kwenye Makumbusho yanapata mapato makubwa na kujenga uchumi wa nchi husika hivyo akaelekeza watendaji waige huko ili makumbusho ya Taifa yachangie kwenye uchumi wa nchi yetu.
"Angalieni wenzetu wanafanya nini kwenye mataifa mengine yaliyoendelea duniani, hasa katika taifa kama Singapore ambao hawana wanyama lakini watu wanakwenda kuangalia makumbusho yao na kuingiza fedha nyingi za kigeni". amesisitiza Mhe, Mchengerwa
Aidha, Mhe. Mchengerwa ameitaka Menejimenti ya Makumbusho ya Taifa kuandaa mipango madhubuti ya ujenzi wa Makumbusho ya kisasa itakayovutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kutembelea.
Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na raslimali nyingi za asili ambazo ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya Utalii.
Ameelekeza kupitishwa kwenye Kamati inayoratibu urejeshwaji wa masalia ( Mafuvu) ya machifu yaliyotwaliwa na wakoloni ( wajerumani) kukutana nayo na kukamilisha zoezi hilo ili watanzania wanufaike na raslimali zao kama ulivyoagizwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mchengerwa alipitishwa kwenye Mpango Mkakati wa Taasisi hiyo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Noel Lwoga ambapo alipongeza kwa kuandaa Mpango huo na kuwataka uboreshwe zaidi ili uendane na hali ya sasa.
Wakati huo huo Mhe. Mchengerwa aliishukuru Serikali ya China kupitia balozi wa China hapa nchini, Mhe.CHEN Mingjian kwa msaada wa kusimika sanamu ya Baba wa Taifa katika Ofisi ya Makumbusho ya Taifa na msaada walioutoa wa zaidi ya Dola za kimarekani milioni moja zitakazosaidia kukabiliana na majanga mbalimbali yanayojitokeza kama moto kwenye Wizara hiyo.
Aidha amemshukuru Mhe, Balozi kwa uhusiano mzuri baina uliojengeka baina ya Tanzania na China na kumwomba ashawishi watalii wengi kutoka China waje kutembea Tanzania.
"Na nimemwomba Mhe. Balozi atusaidie katika Ile idadi ya watalii ambao ni takribani milioni 150 wanaotoka China kwenda duniani kutalii basi Tanzania waje angalau milioni tano" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Social Plugin