MCHUNGAJI KIMARO ASAMEHEWA


Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa leo Jumapili ametangaza msamaha kwa Mchungaji wa Ushirika wa Kijitonyama, Dk Eliona Kimaro ambaye alipewa likizo ya siku 60.


Usiku wa Januari 16, 2023 ilisambaa video ikimuonyesha mchungaji Kimaro akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.


Likizo hiyo ilikuwa inamalizika Machi 17, 2023 na Mchungaji Kimaro alipokuwa akiwaaga Washirika wa Kijitonyama alisema baada ya likizo hiyo hatarudi hapo, alielezwa akaripoti Makao Makuu ya Dayosisi.


Katika msamaha huo wa leo Februari 19, umetangazwa katika Ibada iliyofanyika Ushirika wa Kinyerezi, Tabata na kuongozwa na Askofu Malasusa ambapo ametangaza uamuzi huo Kanisani baada ya Mchungaji Kimaro kupewa fursa ya kuwasalimia waumini na akaomba radhi kwa yote yaliyotokea.

"...Mchungaji Kimaro kama ulivyoomba umesamehewa, endelea kutafakari, endelea kukaa karibu na Mungu wako," amesema Askofu Malasusa huku akiwaomba waumini washirika mbalimbali kuwatunza na kuwaombea wachungaji wao.


Akizungumza wakati wa ibada hiyo Mchungaji Kimaro ameomba radhi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote uliojitokeza wakati huu ambao amekuwa likizo.

“Naomba radhi kwa mkuu wa kanisa Askofu, Dk Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote ambao ulijitokeza katika mitandao na kwenye vyombo vya habari kwa wakati huu ambao nimekuwa likizo ya faragha,” amesema Dk Kimaro.




Pia, amemshukuru Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa kwa upendo na kazi kubwa ya kumtunza kichungaji

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post