Maafisa wa usalama katika kaunti ya Kisumu nchini Kenya wanachunguza mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyeuawa akielekea kwenye mkesha wa matanga.
Elvis Odhiambo alidungwa kwa panga katika kaunti ndogo ya Nyakach mnamo Jumamosi, Januari 4 usiku.
Odhiambo ambaye ni mkazi wa Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Mashariki ya eneo la Kodhoch Magharibi Kaunti ya Homa Bay, alikata roho Jumapili, Januari 5, akikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Homa Bay.
Kulingana na ripoti, Odhiambo alitumia barabara fupi kati ya Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Mashariki na Kaunti Ndogo ya Nyakach kutoroka nyumbani ili kuhudhuria disko hiyo.
Bado haijatambuliwa ni nini kilikuwa chanzo cha vita kati ya mvulana huyo na wanaume wasiojulikana ambao walimvamia.
Chifu wa eneo la Kodhoch Magharibi, Charles Dete alisema kuwa mvulana huyo alipata majeraha mabaya kichwani na tumboni.
Baada ya kumcharanga mvulana huyo kwa panga, wavamizi hao walioonekana kujua alikotoka kwani walimbeba na kumtupa katika kituo cha afya cha kaunti ndogo ya Rachuonyo Mashariki akiwa angali hai.
Hata hivyo, alifariki alipokuwa akikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay.
Mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Okita iliyoko Rachuonyo Mashariki huku polisi wakianzisha uchunguzi.
Via: Tuko News