Monica Patrick (31) Mkazi wa Wilaya ya Itilima Mkoa wa Simiyu amekutwa amefariki dunia kwa kuuawa na kisha mwili wake kutumbukizwa kandokando ya kichaka kilichopo pembezoni mwa ziwa Victoria katika Mtaa wa Kinyangwena Manispaa ya Musoma Mkoani Mara.
Chanzo cha kifo chake kinatajwa kuwa alipewa dawa na mganga wa kienyeji kwa lengo la kumsaidia katika shughuli zake za madini.
Wakizungumza na EATV baadhi ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo ambapo mwanamke huyo ametupwa ndani ya maji baadhi ya wananchi hao wameeleza kuwa mama huyo alikuwa ameenda eneo hilo kwa ajili ya kupata tiba kwa mganga
“Mimi ninavyosikia kuwa huyu mama alikuja kutibiwa na mganga wa kienyeji na alipopewa dawa na huyo mganga alipoteza maisha ndipo akatupwa ndani ya vichaka hivi vilivyopo pembezoni mwa ziwa victoria", amesema Madaraka.
“Huyu mama inasemekana alikuwa amekuja kutibiwa na kufanyiwa dawa ili aweze kupata mali kwenye biashara zake za madini ndipo alipokuja kutibiwa na mganga huyu ambaye ameshikiliwa hapa na wananchi", amesema Catherine.
Mbali na tukio hilo la mwanamke huyo kukutwa katika kichaka hicho akiwa amefariki wananchi wakatoa ombi kwa Serikali kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji taka katika eneo hilo kwani kwa sasa limegeuka kuwa eneo la kutupia maiti.
“Eneo hili limekuwa ni eneo hatarishi kutokana na kuwa na vichaka vingi na mpaka sasa huyu sio mtu wakwanza kuokotwa hapa akiwa amekufa hivyo tunaomba ujenzi wa mradi wa maji taka ukamilike ili vichaka viweze kuondoshwa",amesema Madaraka Jackson.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na uokozi Mkoa wa Mara mrakibu Agustine Magere amesema kuwa walipikea simu ya kwenda kufanya uokozi huku mwenyekiti wa mtaa huo wa kinyangwena akisema haya.
“Katika mtaa wangu hasa katika eneo hili tumeisha shuhudia matukio haya ya watu kutupwa katika vichaka hivi kama mara ya tano kwa hivi sasa na tunashindwa kuelewa watu hawa wanakuwa wanauwawa wapi na kuja kutupwa hapa",amesema Selemani Makanja mwenyekiti wa Mtaa.
CHANZO-EATV