***************
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ametatua mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Ziwa Manyara Mkoani Arusha na wananchi wa kijiji cha Buger kilichopo katika wilaya ya Karatu, uliosababishwa na wananchi hao kuvuka vigingi vya hifadhi na kuendelea na shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
Ametatua mgogoro huo leo wakati wa ziara ya kikazi ya kusikiliza changamoto za wananchi kuhusu mipaka ya hifadhi Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Mhe. Masanja amefafanua kuwa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) baada ya kuweka vigingi katika eneo la kijiji cha Buger, kaya tatu zinaonekana zimo ndani ya hifadhi ambapo awali tathmini ya Kamati ya Mawaziri Nane ilionesha kaya 300 zimo ndani ya hifadhi hivyo kupendekeza kuangaliwa upya uwezekano wa kuziacha kaya hizo.
"Maamuzi ya Baraza la Mawaziri yaliamuliwa na yalitaka baadhi ya kaya ziondoke lakini ikatumwa kamati ya wataalamu uwandani kufanya tathmini upya” Mhe. Masanja amefafanua.
Amesema baada ya kamati hiyo kutoa mapendekezo Serikali iliamua kuweka vigingi kwa lengo la kuzuia wananchi wanaoendelea na shughuli za kibinadamu lakini bado wananchi waliendelea kuingia katika eneo la hifadhi.
Kufuatia uamuzi huo, Mhe. Masanja amesema Serikali italipa fidia kaya tatu zilizo ndani ya hifadhi ya ziwa Manyara baada ya TANAPA kufanya tathmini.
“Niwaombe kwa wale ambao wamevuka vigingi tulivyoweka na kuingia katika hifadhi, Serikali iwalipe fidia baada ya kufanyiwa tathmini”Mhe. Masanja amesisitiza.
Amewaasa wananchi wa kijiji cha Buger kutoendelea kuingia katika eneo la hifadhi ya Ziwa Manyara kwa sababu ndio eneo lenye chanzo cha maji kinachotegemewa na mji wa Karatu na pia husaidia kuhifadhi mazingira na kuchevusha mazao.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dadi Kolimba amesema Serikali inalinda msitu huo kutokana na faida zake katika kuleta mvua na kutunza vyanzo vya maji.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Karatu, Mhe. Daniel Awack amesema ni vyema TANAPA ikaendelea kuimarisha ushirikiano baina yake na wananchi ili waone faida za uhifadhi .
Social Plugin