MTU mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Ismail ambaye aligongwa na Gari la Mwendokasi wakati anatembea kwa miguu kandokando ya Barabara ya Morogoro na Jamhuri, imeelezwa kuwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP. Murilo J. Murilo imeeleza kuwa baada ya kutokea ajali hiyo iliyohusisha Gari mali ya Kampuni ya UDART (Mwendokasi) na Gari ndogo aina ya Toyota Avanza mali ya Rwanda Air, ajali hiyo ilisababisha majeruhi madogo kwa baadhi ya abiria.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa majeruhi wanne wamelazwa katika Hospitali hiyo ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi wakiwemo, Dereva wa Gari ndogo (Toyota Avanza), Jumbe Mohamed (38) na Shukuru Omari (32), Saidi Hasani (43) wote ni abiria gari hiyo ndogo pamoja na mtu huyo ambaye alikuwa anatembea kwa miguu (Ismail).
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na kutojali kwa alama za barabarani kwa Dereva wa gari ndogo aliyekuwa anatoka Mnazi mmoja kuelekea mzunguko wa DTV kutochukua tahadhari wakati anakatisha barabara kubwa ya Morogoro.
Aidha, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa wito kwa Madereva kufuata na kuzingatia Sheria na alama za barabarani kila wakati ili kuepusha ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Ajali hiyo iliyotokea jana Jumatano (Februari 22, 2023) majira ya saa 6:10 katika makutano hayo ya barabara ya Morogoro na Jamhuri, Kisutu, jijini Dar es salaam ikihusisha Gari namba T122 DGW Aina ya Dragon mali ya Kampuni ya UDART (Mwendokasi) na Gari ndogo aina ya Toyota Avanza, mali ya Rwanda Air.
Chanzo- Michuzi TV
Social Plugin