SERIKALI YATOA MSIMAMO WAKE KWA WADAU WA UTANGAZAJI NCHINI



Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akifungua Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma wa Sekta ya Utangazaji Tanzania  katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Bakari akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma wa Sekta ya Utangazaji Tanzania  katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Kauli mbiu ni Mchango wa Sekta ya Utangazaji katika kukuza uchumi wa kidigitali
Mkutano wa Mwaka wa Watoa Huduma wa Sekta ya Utangazaji Tanzania 

Na Dotto Kwilasa, Malunde1 Blog-DODOMA.

IKIWA ni siku ya Radio duniani, Serikali imesema ipo tayari wakati wowote kushirikiana na wadau utangazaji katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora kisera na kibiashara katika uwezeshaji na utoaji huduma bora nchini.


Kwa kudhihirisha hilo imechukua hatua mbalimbali kutatua changamoto za kiuchumi katika vituo vya utangazaji nchini kwa kupunguza ada za leseni za mwaka kwa takribani asilimia 40 pamoja na ada za masafa ya utangazaji katika maeneo yasiyo tija kibiashara.


Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknoloji ya habari  Mhandisi Kundo Mathew amesema hayo leo Februali 13,2023 jijini hapa wakati akifungua Mkutano wa  siku mbili wa mwaka wa Watoa huduma wa Sekta ya Utangazaji pamoja na Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani.


Amesema hatua hiyo ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuhakikisha kwamba huduma za utangazaji zinaboreshwa.


"Sekta ya utangazaji imekuwa ikipitia mabadiliko ya kiteknolojia ambayo kila wakati yanahitaji marekebisho , historia ya redio na runinga nchini kwa takribani miaka 50 utangazaji wake ulitumia mitambo ya analojia. Kwa runinga hadi mwaka 2010 nchi ilihama kutoka kutumia mitambo ya analojia na kwenda kidigiti,"amesema.


Siku ya Redio, amesema siku hiyo huadhimishwa chini ya Mwamvuli wa Shirika la Umoja wa Mataifa Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Chimbuli la siku hiyo linatokanana mkutano wa 36 wa UNESCO uliofanyika Novemba 3, 2011 na kuanza kuandhimishwa rasmi 2012.


Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari amesema ikiwa ni siku ya Redio duniani, mamlaka hiyo bado inatambua kuwa Radio ni mawasiliano ya umma ambayo yanawafikia kundi kubwa la wasikilizaji ulimwenguni kote.


Amesema TCRA bado inatambulika kuwa ni chombo cha mawasiliano chenye nguvu ya ushawishi na kinatumia gharama ndogo na nafuu zaidi katika kujiendasha .


"Tafiti mbalimbali zinaonyesha  radio iliandaliwa kuzifikia jamii zilizo katika maeneo yaliyoko kando ya miji na vijiji, ambavyo haviwezi kufikiwa kwa urahisi kutokana na matatizo ya barabara na usafiri,jamii ambazo zinaathirika zaidi na matatizo mbalimbali kama vile, waliokosa fursa za elimu, wenye ulemavu, wanawake, vijana na maskini na utambuzi wa fursa", amesema.


Amesema hadi sasa nchini kuna jumla ya watoa huduma za mawasiliano 787 ambapo vyote kwa pamoja vinasaidia kuleta mchango wa sekta ya utangazaji katika kukuza uchumi wa kidigitali.


"Mamlaka yetu ya TCRA yenye sekta za mawasiliano, utangazaji pamoja na posta na usafirishaji tunaendelea kusimamia vyombo vyote vya habari katika kútoa maudhui sahihi yanayoendana na utamaduni wetu kwa kuwa tunaelewa vyombo vyote vina mchango kwenye jamii",ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post