Na Dotto Kwilasa, Malunde I Blog,DODOMA.
SERIKALI imetoa jumla ya shilingi bilioni 54.2 kwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni Dodoma ambapo mradi huo uliwekwa jiwe la msingi na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango Novemba 30 mwaka jana.
Hayo yamebainishwa jijini hapa na Mtendaji Mkuu wa TBA Daud Kondoro wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa wakala huo katika kipindi cha miaka miwili.
Licha ya hayo amesema Serikali itaendelea kuiwezesha TBA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni Pamoja na kutoa fedha za ruzuku kwa ajili ya kutekeleza miradi ya serikali. katika kipindi cha miezi 18 na kwamba tayari imetoa sh. bilioni 54.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
Amefafanua kuwa serikali imeshatoa sh.bilioni 15.5 kwa kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 150 ambao umefikia asilimia 81 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 za awamu ya pili ukiwa umefikia asilimia tatu.
“Mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za viongozi jijini Dodoma ambao umegharimu sh.bilioni tisa mradi huu ulitekelezwa ili kukabiliana na uhaba wa nyumba za makazi ya viongozi uliojitokeza mara baada ya serikali kuhamishia makao yake makuu jijini Dodoma mradi huu umeshakamilika kwa asilimia 100,”amesema.
Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma katika eneo la magomeni kota, awamu ya kwanza na ya pili ambao unagharimu sh.bilioni 7.8 ambapo ujenzi wa jengo la ghorofa nane lenye uwezo wa kuchukua familia 16 tayari limeshakamilika kwa asilimia 99.
Amebainisha kuwa katika ujenzi wa awamu ya pili jengo la ghorofa nane umefikia asilimia 25 huku mradi mwingine wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Temeke Kota ukiendelea ambapo linajengwa jengo la ghorofa tisa linalochukua familia 144.