VIJANA 170 WAPATA MAFUNZO YA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA


Kamishina wa Mafuta na Gesi Michael Mjinja akikata utepe kuzindua mafunzo tarehe 15, 2023 katika chuo cha Veta mkoani Tanga kwa ajili ya Watanzania 170 wanaopewa mafunzo ya kusimamia usalama, uhifadhi wa mazingara na afya za wafanyakazi wa mradi wa bomba la mafuta (EACOP) linalojengwa kutoka Hoima Uganda mpaka kijiji cha Chongoleani mkoani Tanga.Sehemu ya vijana wa Kitanzania waliopatiwa mafunzo kwa ajili ya miradi wa bomba la mafuta ( EACOP) 

****************** 

*Mafunzo ya vijana hao yana hadhi ya Kimataifa 

Na Mwandishi Wetu 

Serikali imepongeza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa kuwapatia mafunzo yenye hadhi ya kimataifa Watanzania wapatao 170 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa bomba hilo la mafuta unaotegemewa kuanza kati kati ya mwezi huu. 

Maeneo hayo waliopatiwa mafunzo Watanzania hao ni katika sekta ya kusimamia afya , usalama wa wafanyakazi wakiwa kazini na utunzaji wa mazingira katika maeneo yote yanayohusu mradi. 

Bomba hilo la mafuta linajumlisha eneo lenye jumla ya kilomita 1,443 kutoka Kabaale, Hoima nchini Uganda mpaka katika kijiji cha Chongoleani kilichopo Tanga. 

Akizungumza mkoani Tanga Februari 15, 2023 wakati wa kuzindua mafunzo hayo ya kuwaongezea ujuzi na maarifa Watanzania 20 kati ya walengwa 170 ambao bado wengine wanaendelea na mafunzo hayo katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) mkoani Tanga na Arusha, Kamishna wa Mafuta na Gesi nchini Michael Mjinja kutoka Wizara ya Nishati na Madini amesema Watanzania hao watakuwa rasilimali muhimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwaletea maendeleo Watanzania. 

Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule wa gesi Asilia ( LNG) ambao uchimbaji wake utafanyika chini ya ardhi na baharini. 

Amesema mradi wa bomba la Mafuta (EACOP) una umuhimu katika maendeleo ya nchi ambapo utaajiri Watanzania wengi na kuwapatia ujuzi kutoka kwa wakandarasi wa kigeni. 

“Mradi huu una manufaa makubwa kwa taifa ambapo mbali na biashara ya mafuta, ajira nyingi zinatengezwa na wataalam wazawa kuzalishwa kwa ajili ya miradi mingine ya kimkakati,” amesema.

Hata hivyo amesema kuwa mradi huo umezingatia viwango vya kimataifa na kuwataka wananchi kupuuza upotoshaji wa mradi huo kuwa hauzingatii viwango vya kimataifa.

Na badala yake amesema mradi huo unazingatia matakwa yote na ni rafiki katika utunzaji wa mazingira. 

Pia amesema mradi umezingatia haki za waathirika wa maeneo yanayopita mradi huo ambapo wale ambao maeneo yao yameguswa ikiwemo nyumba zao kuondolewa wanalipwa fidia kwa kufuata muongozo wa sheria za nchi. 

Lakini pia amesema mradi huo umekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo wazawa wa maeneo husika kupata ajira. 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Uwezeshaji Watu wa EACOP, Martha Makoi, katika utekelezaji wa mradi huu, kila mkandarasi ana kipengele kinachomtaka kuwapa mafunzo wafanyakazi wazawa katika jinsi zote ( kike na kiume) ili kuzalisha wataalamu na kuwajengea uwezo ili watumike baadae katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya nchi endapo wakandarasi wageni wataondoka pindi miradi itakapokamilika. 

Amesema ndio maana jumla ya Watanzania 170 watapewa mafunzo hayo ambapo tayari 20 kati ya hao wamehitimu katika chuo cha Veta mkoani Tanga, huku wengine 25 wakiendelea na mafunzo yao katika chuo cha hicho mkoani Arusha. 

Lengo la mafunzo hayo yanayojulikana kama H3SE ni kupewa mbinu za kuzuia ajali zinazoweza kutoka katika mradi na kuhatarisha usalama wa wafanyakazi. 

Lakini pia kuhakikisha mazingira yanayopita mradi yanaendelea kutunzwa katika uasili wake bila uharibifu wowote na kuhakikisha afya za wafanyakazi zinakuwa bora kwa ajili ya kuwajibika zaidi. 

Mmoja wa wahitimu hao, Sabrina Salim mwenye Shahada ya Mazingira aliyoipata kabla ya kupewa mafunzo haya amesema kauli yao mbiu wakati wa mafunzo na itakayotumika katika eneo la mradi ni ‘ Usalama Kwanza- Safety First’. 

Amesema anajivunia kuwa sehemu ya mafunzo hayo na mbali ya elimu ya mazingira aliyokuwa nayo kabla, kupitia mafunzo haya amepewa mafunzo ya ziada juu ya kusimamia usalama wa wafanyakazi na utunzaji wa mazingira katika ubora wa kimataifa. 

Kwa mujibu wa Martha Joash Makenge kutoka kampuni ya Daqing Oilfield Construction Group Co. Limited, iliyopewa kazi ya Ukandarasi wa kujenga matenki na sehemu za kuhifadhia mafuta, mafunzo haya hutolewa kwa ushirikiano na chuo cha Veta cha Moshi na Arusha na hutambulika kimataifa. 

Amesema kuelekea utekelezaji wa mradi huo, tayari kazi ya awali , ikiwemo kusafisha maeneo mradi utakaopita na kuwalipa wananchi wanaopitiwa na zoezi hilo la ujenzi wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1443 kutoka Kabaale, Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani mkoani Tanga. 

Amesema mradi wa ujenzi wa bomba hilo la mafuta unatarajiwa kuanza kati kati ya mwaka huu kwa kipindi cha miaka 3-4. 

Asiadi Mrutu, Mratibu wa mradi wa EACOP kutoka Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) amesema maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa bomba, ambalo limegusa ajira za zaidi ya Watanzania 1672 yamekamilika. 

Amesema jumla ya watu 9508 watalipwa fidia kwa kupitiwa na mradi huo, ambapo 8922 ( zaidi ya asilimia 93) wamekubali kupokea fidia hiyo na tayari watu 8450 wameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 29 za Kitanzania kama fidia na kupewa notisi za kuhama maeneo yao ifikapo mwezi Mei mwaka huu ili kupisha ujenzi. 

Julien Bouwense, Meneja wa Bandari ya Mafuta inayojengwa katika kijijini cha Chongoleani mkoani Tanga amesema ni matumaini yake kuwa Watanzania na Waganda watafurahia zaidi matunda ya mradi huo pindi utakapokamilika. 

Amesema miongoni mwa faida zitakazopatikana ni kupatikana kwa watalaamu wazawa ambao watakuwa na uwezo wa kusimamia miradi mikubwa hapo baadae na uzalishaji mkubwa wa ajira. 

Neema Mwakatobe, Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Ushiriki wa Watanzania kwenye Miradi kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ameusifu mradi wa EACOP kwa kuwapatia Watanzania mafunzo hayo muhimu kupitia mradi huu mkubwa wa kimkakati. 

Amesema kupitia mradi huu, Watanzania wanapatiwa elimu na ujuzi wa teknolojia (Technology Transfer) utakaokuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa hapa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post