Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATANZANIA WATAKIWA KUWA SEHEMU YA UOKOZI KWENYE MAAFA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi nakala za Nyaraka za Usimamizi wa Maafa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula baada ya kuzindua nyaraka hizo kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose, Senyamule. (OPicha na Ofisi ya Wziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua  Nyaraka za Usimamizi wa Maafa kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwa katika picha ya pamoja na Skauti  baada ya kuzindua Nyaraka za  Usimamizi wa Maafa kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023.  Kushoto kwake ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose, Senyamule. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

 Na Dotto Kwilasa, Malunde I Blog-DODOMA.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amezindua nyaraka za usimamizi wa maafa huku akiwataka watanzania wote kuwajibika na kuwa sehemu ya uokozi pindi maafa yanapotokea.

Ameyasema hayo leo Alhamisi, Februari 9, 2023 jijini hapa kwenye uzinduzi wa nyaraka za usimamizi wa maafa ikiwemo mkakati wa Taifa na usimamizi wa maafa,mpango mkakati wa Taifa wa afya Moja na mpango wa Taifa wa mawasiliano wakati wa maafa.

Akiongea  wakati wa uzinduzi huo,Waziri Majaliwa amesema pindi maafa yanapotokea sekta zote zinapaswa kuwajibika na kusisitiza wanaohusika na usimamizi wa maafa watekeleze majukumu yao ipasavyo.

 Pamoja na hayo amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.

Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.

"Kuwepo Kwa miongozo na mipango ya usimamizi wa maafa kutatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza,"amesema 

Ameeleza kuwa Tanzania bado ina uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo pia  kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali  itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.

Katika kufanikisha hayo amezielekeza wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao.

 “Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com