Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao na waandishi wa Habari Februari 7, 2023 kuhusu Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa utakaofanyika Februari 9, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano Kambarage Hazina Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa pamoja na Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.
******************************
Na Mwandishi wetu; Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Uzinduzi wa Nyaraka za Usimamizi wa Maafa nchini tarehe 09 Februari, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage uliopo Hazina Jijini Dodoma.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene alipokutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya habari Bungeni Dodoma tarehe 7 Februari, 2023 kwa lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu tukio la uzinduzi.
Waziri Simbachawene alisema, katika kuendeleza juhudi za kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa Nchini, Serikali imefanya mapitio ya Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2012), Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2012) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2015-2020). Hivyo, mapitio hayo yamewezesha kuandaliwa kwa nyaraka tano zitakazozinduliwa ikiwemo;Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022),Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa (2022) na Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027),Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).
“Nyaraka zote tano zimeandaliwa kwa kushirikisha wadau ndani na nje ya Serikali. Nyaraka zinazozinduliwa zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na baadaye katika mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa,”alisema Waziri.
Alifafanua kuwa, mipango na mikakati iliyoandaliwa itaimarisha usimamizi wa maafa yanayosababishwa na majanga ya nguvu za asili kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi na majanga yanayochochewa na shughuli za kibinadamu.
Aidha, Majukumu ya utendaji yanazingatia taasisi yenye wajibu wa kisheria, ujuzi pamoja na rasilimali zinazohitajika. Mfumo uliopo umezingatia wajibu wa sekta kutambua hatari za maafa katika eneo lake, kutenga rasilimali za kisekta kabla ya tukio kwa ajili ya kuzuia au kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabili maafa endapo yatatokea.
Aliongezea kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuimarisha shughuli za kuratibu na kusimamia shughuli za maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na Kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na miongozo, mikakati na taratibu za kiutendaji zinazowezesha utekelezaji wa majukumu na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano wa wadau.
Social Plugin