Wanawake marafiki wa Samia (Friends Of Samia) kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini, wamejumuika kupata mlo wa Pamoja katika Mgahawa wa Shishi (Shishi Food) uliopo Jijini Dar es salaam, ikiwa ni kuadhimisha kutimiza miaka 2 ya Uongozi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan sambamba na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Wanawake wapambanaji.
Wakielezea Jumuiko hilo wanawake hao wa Friends Of Samia, wakiongozwa na Mbunge wa Mkoa wa Singida Martha Gwau wamesema kwa pamoja wanatambua kazi inayofanywa na Rais Samia ambaye jana Machi 19, 2023 ametimiza miaka 2 tangu awe Rais huku wakitumia nafasi hiyo kumuahidi kuendelea kumuunga mkono kwenye uongozi wake.
"Mama Samia ni mwanamke mwenzetu ametuheshimisha ametuonesha Wanawake tunaweza, 2025 ushindi ni lazima na sisi Wanawake tunamuunga mkono tunamshukuru na tunampenda" ,amesema Mbunge Martha Gwau.
Aidha wanawake hao wameelezea sababu ya kukutana kwao kwenye Mgahawa wa Shishi Food kuwa ni kuishi kwa vitendo kauli ya Rais Samia kuhusu wanawake kupendana na kushirikiana, hivyo wao waliamua kwenda kuonesha upendo kwa Msanii Shilole kwa kupata chakula cha pamoja kwenye Mgahawa wake.
"Tunamshukuru sana Shishi na Wanawake Wachapakazi aina ya Shishi, lazima tuwaunge mkono, kwa sababu ni mfano wa Wanawake wote" ameeleza Mbunge Martha Gwau
Kwa upande wake Shilole, amewashukuru wanawake hao wa Friends Of Samia, akiwaomba waendelee kueleza mambo mazuri yanayofanywa na Rais hasa kwenye kuwaletea maendeleo Watanzania.
"Nina furaha sana mmekuja kunisapoti Shishi Food, sisi wote ni Friend Of Samia Suluhu Hassan, na sijui tulichelewa wapi kumpata Mama Samia, mimi mwenyewe namshukuru binafsi kwa sababu anawainua wanawake wenzake, na 2025 tutakua na Mama yetu Samia Suluhu Hassan" Amesema Shilole huku akionesha kuwa mwenye furaha isiyo na kifani.