Mchungaji mmoja kutoka nchini Uganda amefunga kanisa lake baada ya kushinda zaidi ya KSh5.4 milioni (Milioni 100 za Tanzania) kwenye mchezo wa bahati nasibu (betting).
Machi 16, mwaka huu mtandao mmoja Uganda ulichapisha taarifa za mchungaji huyo akieleza kuwa ameamua kufunga kanisa lake ili afanye shughuli nyingine kwa kuwa amepata fedha nyingi.
Mtandao huo ulimnukuu mchungaji akieleza namna alivyocheza bahati nasibu ya Sh1 milioni lakini akashinda Sh100 milioni ambazo hakutarajia kama angepata.
Kwa mujibu wa taarifa ya vyombo vya habari nchini humo, mchungaji huyo aliamua kufunga kanisa lake ili afanye shughuli nyingine kwa sababu sasa ni tajiri.
Alikiri kuwa alifungua kanisa hilo kwa sababu ya tamaa na wala sio upako.
“I must admit that I opened this church due to greed but not anointing (lazima nikiri nilifungua kanisa hili kwa sababu ya ‘kiroho’ lakini sio upako) inasema sehemu ya habari hiyo ikimnukuu mchungaji huyo.
Mchungaji huyo aliongeza kuwa alilazimika kufunga kanisa kwa sababu alikuwa na njia zake za kupata pesa na kufikia sasa amefanya mambo mengi ambayo hakuwahi kufikiria kama angeweza kuyafanya maishani mwake.
Maoni ya viongozi wa kidini kuhusu tukio hilo
Sakata hilo limezua hisia mseto miongoni mwa viongozi wa kidini nchini humo.
Baadhi ya viongozi wa dini walisema kuwa kuna wachungaji wengi wanaofanya mambo kama hayo.
Askofu mmoja alisema kitendo cha pasta huyo kinathibitisha hakuwa amechaguliwa kuwatumikia waumini, bali alitaka kujinufaisha kifedha.
Aliwashauri waumini wachague watumishi wa Mungu kwa kuwapima, vinginevyo yatakuja kutokea majanga.
“Kwanza mtu wa Mungu kucheza kamari sio kitendo chema, lakini Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao sio maneno na huyo alishakuwa mtu wa namna hiyo,” alisema Askofu Anthony Mlyashimba anayehudumu katika Kanisa la Baptist.
“Huyu angeweza hata kuiba ilimradi tu apate fedha, hii sio sawa kwangu mimi hata kidogo, lazima tuwatambue watu wa namna hii na waumini wetu wawe makini sana,” alisema kiongozi mwingine wa kidini.
Social Plugin