Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdul Rahman akizungumza na wananchi Kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya magari ya Pangani kuhusiana na mambo mbalimbali ya kuleta maendeleo jijini Tanga
Na SALMA AMOUR - TANGA
Chama Cha mapinduzi CCM mkoa Tanga kimewataka wananchi kutoilaumu serikali kuhusiana na hali ngumu ya maisha ambayo ndiyo kilio kikubwa kwa wananchi wengi kwa sasa na kuwataka kumtegemea mungu kwa kufanya kazi kwa bidii Ili waweze kufikia lengo.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya Pangani kata ya Msandweni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdul Rahmana ameeleza kuwa serikali ipo kwa ajili ya kutekeleza mahitaji ya wananchi wote ili kuleta maendeleo kwenye jamii na taifa kwa ujumla.
"Kuna watu wakikaa kuanzia asubuhi mpaka jioni kazi yao ni kukilaumu Chama Cha Mapinduzi kwa hali ngumu ya maisha bila kufikiria kuwa hali hii pia inasababishwa na mambo maovu yanayoendelea kwenye jamii. Jamani mfano kuna watu wanamlaumu Rais Samia kuwa mvua hainyeshi , Rais sio anayeleta mvua ni Mungu tufanyeni ibada ili kupata nafuu ya maisha", amesema.
Katika hatua nyingine ameelaea kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutoa ushirikiano kwenye jamii ili kuleta maendeleo katika idara mbalimbali ikiwemo suala ya upatikanaji wa huduma ya maji, umeme na huduma ya afya ili wananchi waweze kupata huduma kuhusiana na shughuli zao za kila siku.