Basi la shule
Wizara ya Elimu imepiga marufuku kuwekwa kwa miziki, nyimbo ama picha za video zinazokwenda kinyume na maadili, mila, desturi na tamaduni katika mabasi yanayotumika kusafirisha watoto kuwapeleka shule, badala yake ziwekwe nyimbo au video zenye kujenga maadili na uzalendo kwa wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa, na kusema kuwa wamiliki wote wa shule wenye kutoa huduma za usafiri kwa wanafunzi pia wahakikishe vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wakiwa kwenye magari au mabasi vinakomeshwa.
Aidha Wizara ya Elimu pia imewataka wamiliki hao kuhakikisha kwamba magari au mabasi yao yanayotumika kusafirisha wanafunzi yanakuwa na vioo angavu na sio tinted.
Waraka huo umelenga kuboresha huduma za usafiri wa mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi wakati wa kurudi ama kwenda shuleni, kufuatia uwepo wa watoa huduma katika magari hayo kuwa na tabia za viashiria vya kuleta mmonyoko wa maadili, kuathiri ukuaji, ujifunzaji na kuhatarisha ustawi wa watoto kiujumla.
Ikumbukwe hivi karibu kupitia mitandao ya kijamii ilisambaa video fupi ikionesha watoto wadogo waliokuwa kwenye gari la shule wakiimba nyimbo ambazo hazileti afya nzuri katika ukuaji na ustawi wa maadili kwao.
CHANZO - EATV