Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza kwenye kambi ya wazee wa Kolandoto.
Na Marco Abel, Shinyanga
MTANDAO wa polisi wanawake mkoa Shinyanga wamefanya matembezi na kutoa msaada wa chakula na vitu mbalimbali kwenye kituo cha makazi ya wazee na wasiojiweza kilichopo kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga.
Mtandao huo umetoa msaada tarehe 07/03/2023 katika maadhimisho kuelekea siku ya wanawake duniani ifikapo Machi 8 mwaka huu kwenye kituo cha malezi ya wazee wasiojiweza, Kolandoto mkoani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake mkoa wa shinyanga ambaye pia ni kamanda wa polisi mkoani humo ACP Janeth Magomi amesema wameamua kutoa msaada huo ili kuonyesha upendo na kuwathamini wazee hao kwani kwa kufanya hivyo inawatia moyo na kuona namna serikali na watu wengine wanavyothamini uwepo wao.
“Kuelekea siku ya wanawake duniani sisi kama mtandao wa polisi wanawake mkoa wa Shinyanga tumeona tufike kwenye kituo cha malezi ya wazee wasiojiweza ili kuonyesha thamani yao kwetu na kutambua uwepo wao, tumefurahi kujumuika nanyi siku ya leo”, ameseam Magomi.
Mratibu wa kituo cha makazi ya wazee na wasiojiweza Kolandoto Sophia Kang’ombe amesema wameendelea kutoa huduma za malazi, chakula na matibabu kwa wazee hao licha ya idadi yao kupungua.
“Kipindi cha nyuma tulikuwa na idadi kubwa ya wazee lakini kutokana na jitihada za serikali kuwaunganisha wazee hawa pamoja na ndugu zao hadi sasa wameweza kupungua na kufikia wanaume 11 na wanawake 5”, amesema Sophia Kang’ombe.
Naye mwenyekiti wa makazi ya wazee kituo cha kolandoto Kija Nipuge amewashukuru Mtandao wa polisi wanawake mkoa Shinyanga kwa kuwatembelea na kutoa msaada kituoni hapo na kuomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono kitu hicho.
Social Plugin