Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALOZI POLEPOLE AKABIDHI MSAADA KWA SERIKALI YA MALAWI

Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo baada ya kuwasilisha misaada ya Kibinadamu iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje Nchini Malawi Mhe. Nancy Tembo akipokea msaada wa unga kutoka kwa Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole wakati wa kukabidhiwa misaada Kwa Wahanga wa Kimbunga Freddy.

 
Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo, Watendaji idara ya Menejimenti ya Mafaa ya Tanzania na Malawi na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania watakao shiriki katika Operesheni kusaidia Wahanga wa Kimbunga Freddy.


Na Mwandishi wetu, MALAWI.

Balozi wa Tanzania Nchini Malawi Mhe. Humphrey Polepole ameshiriki katIka zoezi la kukabidhi misaada ya Kibinadamu kutoka Tanzania kwa Serikali ya Malawi ili kusaidia wahanga wa Kimbunga Freddy.

Balozi amekabidhi misaada hiyo ya kibinadamu inayojumuisha Mablanket, Mahema, Unga wa Mahindi kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi Mhe. Nancy Tembo katika Mji wa   Blantrey Nchini Malawi mapema leo 25/03/2023.

Akikabidhi msaada huo Polepole amesema watanzania, na watu wa Malawi ni jamii moja, na Nia ni kuendekeza umoja uliojengwa na waasisi wa Nchi zetu.

 " Msaada huu wa kibinadamu  utasaidia, katika jitihada za kurejesha matumaini na ustawi kwa ndugu zetu Wananchi wa Malawi", Alisisitiza Balozi Polepole.

Ameongeza kusema kuwa ana imani na wapiganaji  wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioenda  Nchini Malawi  watashirikiana na wenzao Wanajeshi wa Malawi, kuhakikisha kwamba misaada iliyotolewa inawafikia  Wahanga wa Kimbunga Freddy.  

Aidha, Tanzania imetoa madawa ya binadamu, ambayo yataweza kusaidia kwenye maeneo ambayo vituo vya afya vimeathirika. Hizi zote ni jitihada za kusaidia Nchi ya Malawi katika kurejesha huduma za afya.

 

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Msaada aliotoa kwa Nchi ya Malawi, kwa uwezeshaji wa fedha na wapiganaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (Wahandisi wa Medani) ambao watasaidia katika kurejesha hali ya miundo mbinu Nchini Malawi," amesema Balozi.

 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje wa Nchi ya Malawi Mhe. Nancy Tembo amesema ameshukuru Nchi ya Tanzania kwa Msaada wa kibinadamu iliowapatia, ambao umefika katika wakati muafaka.

“Msaada huu ni muhimu kwetu kwa sababu tunao Wanachi wengi ambao makazi yao yameharibika, na tunahitaji msaada wa kila mtu ili kuhakikisha wahanga wa Kimbunga Freddy wanapatiwa huduma za msingi kwa wakati,” alisema Waziri Nancy

Ameongeza kusema Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wamekuja kutusaidia na wataungana na askari wetu wa Nchini Malawi katika kurudisha miundo mbinu iliyoharibika katika hali ya kawaida.

“Nachukua fursa hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutusaidia katika wakati ambao tunahitaji msaada sana, janga hili ambalo limeathiri Nchi ya Malawi, limegharimu maisha ya watu, na limeharibu miundo mbinu” amesema Waziri Nancy.

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulika na Operesheni pamoja na Uratibu wa shughuli za Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu Luteni Kanali Selestine Masalamado ametoa pole kwa wananchi wa Malawi kwa Maafa ya Kimbunga Freddy.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maafa kuratibu swala la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Wahanga  wa Kimbunga Freddy Nchini Malawi, ambapo kwa awamu ya kwanza helikopta mbili kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania zilisafiri kuja Malawi kufanya kazi za wokozi,  lakini msaada wa pili ilikuwa ni msaada wa fedha kwa serikali ya Malawi na tatu ni kutoa msaada wa kibinadamu kwa Wahanga wa Kimbunga Freddy.

 

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com