Katika siku za hivi karibuni, wanaume wamekuwa wakikimbia kortini kuwashtaki wanawake ambao wamekuwa wakiwakwepa baada ya kuwatumia nauli.
Hususan katika kaunti ya Uasin Gishu idadi ya wanaume waliokuwa wakilalamika wapenzi wao kula 'fare' imekuwa ikiongezeka. Lakini mahakama ni kama imechoshwa na kesi hizo.
Hata hivyo, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Eldoret anayeshughulikia kesi ndogo mjini humo, Tabitha Wanjiku Mbugua alisema kuwa korti yake haina mamlaka ya kuwashurutisha wanawake wanaokula nauli za wapenzi wao kuzirejesha.
Akizungumza Jumapili, Februari 26, katika hafla ya kutoa shukrani iliyoandaliwa na idara ya polisi, aliwashauri wanaume kutowatumia wanawake nauli.
"Ninawahurumia wanaume wanapoteza pesa zao kwa wapenzi wao wa kike kwa kuwatumia nauli. Inashangaza kwamba wapenzi hao wanakula wanakula nauli lakini wanakosa kwenda."
"Baadhi ya wanaume wamefika katia korti yangu na kutaka usaidizi ila kwa bahati mbaya korti yangu haina uwezo wa kuwashurutisha wanawake kurejesha pesa hizo. Mahakama ya kushughulikia madai madogo madogo haina mamlaka ya kushughulikia kesi hizo," alisema hakimu huyo kama alivyonukuliwa na gazeti la Taifa Leo.
Hakimu Wanjiku pia aliwaonya Wakenya wenye mazoea ya kwenda kwa waganga ili kurejeshewa pesa zao akisema juhudi zao zitafeli. Wanjiku alieleza kuwa korti haiwatambui waganga hao.
Chanzo- Tuko News