Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya uchunguzi kupasuka kwa bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui afanya kikao na uongozi wa Mgodi huo kufuatilia hatua za ulipwaji fidia wananchi,
Na Ofisi ya habari Kishapu.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkunde ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi kuvunjika kwa kingo za bwawa la maji tope katika mgodi wa almasi Mwadui (Williamson Diamond Limited) uliopo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, amefanya kikao na uongozi wa mgodi huo ili kufahamu hatua ya ulipaji wa fidia waliyofikia tangu kupasuka kwa bwawa hilo Novemba 7 mwaka jana.
Awali akitoa taarifa wakati wa kikao hicho jana Machi 21,2023, Afisa Uhusiano wa Mgodi huo Benard Mihayo, amesema tayari timu yao imeshafanya tathimini na kubaini waathiriwa wanaostahili kulipwa fidia na kujengewa nyumba kufuatia tope la mgodi huo kuharibu makazi na mashamba ya wakazi wa Vijiji vya Ng'wanholo na Nyenze vilivyopo Kata ya Mwadui Luhumbo kwa kufunikwa na tope.
“Tathimini imefanyika na kubaini makundi yanayostahili kulipwa fidia kuwa ni pamoja na wamiliki wa ardhi, wapangaji, waliokuwa wamekodisha mashamba pamoja na waliopoteza mifugo na tayari tumeanza ulipaji wa fidia na mpaka sasa ulipaji upo Asilimia 18 na waathirika wengine tunaendelea kuwafungulia akaunti za benki ili tuweze kuwalipa stahiki zao,” amesema Mihayo.
Kwa upande wake Meneja wa Mgodi huo, Ayoub Mwenda ameishukuru tume ya madini na Serikali kwa kuendelea kuwapa ushirikiano katika kuhakikisha waathiriwa wote wanalipwa fidia kwa kuzingatia sheria na miongozi ya Serikali.
“Tunaishukuru tume ya madini kwa kuendelea kushirikiana nasi ambapo Machi 6 mwaka huu tumepata kibali cha kuendelea kujenga bwawa jipya la Tope hadi sasa ujenzi umefika asilimia 25 na kufikia Julai 2023 tutakuwa tumekamilisha na uzalishaji kuendelea," amesema Mwenda.
Aidha, Mhe. Mkude ameupongeza uongozi wa mgodi huo kwa hatua waliyofika na ameahidi kutoa ushirikiano kila muda kuhakikisha waathirika wa tope wanapata stahiki zao na kuagiza hadi kufikia Machi 31 mwaka huu Waathirika wote wawe tayari wameshalipwa fidia.
“Jitahidini kulisukuma kwa haraka ili waathiriwa waliobakia wapate fidia hadi kufikia tararehe 31 Machi 2023 Waathirika wote wawe wameshalipwa, na mimi nitashirikiana nanyi kila mkihitaji msaada kutoka ofisini kwangu," amesema Mhe. Mkude.
Social Plugin