Na Mwandishi Wetu Michuzi TV
MAANDALIZI ya Tamasha la Pasaka yanazidi kunoga baada ya mwimbaji mwingine mahiri wa nyimbo za Injli nchini, Christopher Mwahangila kuthibitisha kushiriki tamasha hilo linalotarajia kufanyika Aprili 9 mwaka huu kwenye viwanja vya Leaders Club,Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na mamia ya mashabiki na wapenzi wa muziki wa Injili nchini hasa wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa jirani.
Akizungumza leo mbele ya Waandishi wa Habari katika Ofisi za Msama Promotion ambao ndio waandaaji wa tamasha hilo, Mwahangila ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kutokana na nyimbo zake za Injili zikiwemo Mungu ni Mungu,Fungua Milango,Moyo Furahi,Yesu yuko hapa na nyinginezo amesema tamasha la pasaka limekuja wakati muafaka kwani wamelikosa kwa miaka mingi.
Amefafanua miaka saba imepita sasa bila kufanyika tamasha hili, hivyo wanawashukuru waandaaji wa tamasha hilo ambao ni Msama Promotion kwa kulirudisha tena mwaka huu,hakika ni jambo la kumshukuru Mungu huku akisisitiza yuko tayari na amejipanga vema kwa ajili ya tamasha la Pasaka.
“Tamasha la Pasaka litakonga nyoyo za waumini mbalimbali wa nyimbo za Injili na nitaimba 'live' usipange kukosa, lakini pia tujitokeze katika kumpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri aliyoifanya ndani ya miaka miwili, njooni tusifu kwa pamoja,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa matamasha mbalimbali ya Injili nchini, Alex Msama amesema tamasha la mwaka huu litakuwa la kihistoria na kufanyika bure.
Ameongeza maandalizi ya tamasha la Pasaka yanaendelea vizuri na kwamba awali tamasha hilo lilitakiwa lifanyike uwanja wa Taifa, lakini kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao tamasha hilo litafanyika Leaders club.
"Kwa hiyo tamasha lipo kama kawaida Aprili 9, 2023 na mpaka sasa waimbaji wengi wamethibitsha kushiriki" amesema Msama na kuongeza tamasha hilo pia litakuwa la kumshukuru Mungu katika kusherehekea miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.Tutatumia nafasi hiyo kumuombea ili aendelee kuiongoza nchi ya Tanzania kwa amani."
Pia tamasha hilo litakuwa la kumshuru Mungu kwaajili ya uongozi wa mama yetu , Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili madarakani kwa mafanikio makubwa, miradi mingi imeendelea, kila kitu kinaenda vizuri, tunaishi kwa amani na utulivu hivyo ni lazima tumshukru Mungu kwa uongozi wa Rais wetu" ameongeza Msama.
Kuhusu waimbaji ambao watashiriki kwenye tamasha hilo ni pamoja na mwimbaji mahiri wa nyimbo za kusifu na kuabudu Upendo Nkone, kundi la Zabron Singers Emmanuel na wengine wengi ambao wanaendelea kutangazwa.
Wakati huo huo Mratibu wa Tamasha la Pasaka Emmanuel Mabisa amesema waimbaji wote walioalikwa kushiriki kwenye tamasha hilo wamethibitisha ushiriki wao na kwamba maandalizi yote yanaenda vizuri."Tamasha hili lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu.
"Lakini kwa sasa limewadia, hivyo niwaombe wananchi wasisite kutoka na familia zao kuhudhuria kwenye tamamsha hilo vyakula na vinywaji vitakuwepo kwa bei nafuu", amesema Mabisa.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa tamasha la Pasaka kila mwaka Alex Msama (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika bure bila kiingilio April 9, 2023 katika Viwanja vya Leders Club Jijini Dar es salaam.
Mratibu wa tamasha la Pasaka Bw. Emmanuel Mabisa (kulia) akifafanua jambo kuhusu maandalizi ya Tamasha hilo.
Mwimbaji mahiri wa Nyimbo za Injili Christopher Mwahangila (pichani kushoto) akiimba moja ya wimbo wake mbele ya waandishi wa habari kuonesha namna alivyojiandaa kutumbuiza kwenye Tamasha la pasaka linalotarajiwa kufanyika bure katika viwanja vya Leaders Club Kinondoni,Jijini Dar,kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion inayoandaa tamasha hilo kila mwaka Alex Msama, akifurahi jambo.
Social Plugin