Kundi la watalii wapatao 17 kutoka nchini Ufaransa wakiwa katika mgodi wa kuzalisha madini aina ya Tanzanite uliopo katika eneo la kitalu C unaomilikiwa na kampuni ya Franone Mining wilayani Simanjiro Mkoani Manyara
Na Woinde Shizza , ARUSHA
Kundi kubwa la watalii wapatao 17 kutoka nchini Ufaransa wametembelea mgodi wa kuzalisha madini aina ya Tanzanite katika mgodi wa kitalu C unaomilikiwa na kampuni ya Franone Mining iliyopo wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Kundi hilo ambalo ndani yake wapo wataalamu wa kukata na kuongeza thamani ya madini pamoja na wanafunzi wa kuongeza thamani ya madini wamesema wamefurahia kuona sehemu pekee inayochimbwa madini ya Tanzanite mkoani Manyara.
Akizungumza mara baada ya kupokea kundi hilo, Meneja mkuu wa kampuni ya Franone Mining , Vitus Ndakize amesema wamejisikia faraja kubwa kwa wageni hao kufika katika mgodi pekee mkubwa yanapo patikana madini aina ya Tanzanite.
"Kitendo cha hawa watalii kufika kwenye mgodi wetu kimekuwa ni faraja kubwa sana kwani tumeweza kujifunza mengi pia kutoka kwao na tumeweza kuweka historia kwa kutembelewa na kundi hili ambalo wameweza kujionea namna ya utendaji kazi wetu",amesema .
Ndakize ameshukuru Wizara ya Madini kwa kuwakaribisha watalii hao wa sekta ya madini kwani ujio wa wageni hao unaendelea kutangaza nchi ya Tanzania kwamba madini ya Tanzanite yanapatikana pekee nchini Tanzania na sio pengine.
Aidha ameongeza kuwa, kwa sasa mgodi huo umeshaanza kazi rasmi na wanategemea uzalishaji mkubwa kutokana na wataalamu wa miamba kutoka maeneo ambayo madini yanapatikana licha ya mgodi huo kutokufanya kazi kwa muda wa miaka mitano .
Mkuu wa kampuni ya Franone Mining Vitus Ndakize iliyopotea wilayani Simanjiro mkoani manyara akitoa maelezo kwa wageni waliofika kitalu c ,kuangalia namna ya uzalishaji wa madini ya Tanzanite yanavyozalishwa.
"Serikali ilitangaza tenda mwaka 2022 mwezi wa wa nne ambapo kampuni ya Franone Mining ilishinda tenda hiyo mwezi wa sita na kupewa leseni ya uchimbaji mwezi wa saba mwishoni huku serikali ikiwa na ubia asilimia 16 na mpaka sasa umeanza kazi za uchimbaji ikitegemea kuanza uzalishaji wa madini ya Tanzanite wakati wowote ",amesema Meneja .
Kwa upande wake Mmoja wa watalii , Camille Constant kutoka nchini Ufaransa amesema amepata uzoefu wa kipekee wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite hivyo atakua balozi mzuri kwa wenzake pamoja na watalii wengine .
"Nimefurahishwa sana na namna ya uchimbaji wa kisasa ambao unatumika kuchimba na kupata madini ya Tanzanite ikilinganishwa na maeneo mengine walio tembelea katika nchi za Africa kusini , Ivory Cost na Ufaransa kwani nimeona utofauti mkubwa sana katika uchimbaji na nimepata uzoefu wa kutosha pia."amesema Camille.