Mwandishi wetu - Mwanza
Shirika la Tanzania Media for Maritime and Fisheries Development (TMFD) limepokea vilio vya wavuvi katika mwalo wa Mswahili Jijini Mwanza juu ya bei kubwa ya vazi okozi (life Jackets) jambo linalohatarisha usalama wao.
Bwana Jeremia Samwel ambaye ni mvuvi amesema kuna bei kubwa ya vazi okozi na hali hiyo inasababisha baadhi ya wamiliki wa mitumbwi wanashindwa kununua vazi okozi na kupelekea baadhi ya wavuvi kuingia majini bila kuvaa vazi okozi hali hiyo inapunguza usalama wao wakati wa kuendesha shughuli zao za uvuvi.
"Tunaiomba Serikali kuweka punguzo kwenye vazi okozi ili tumudu kununua kwani hii itasaidia usalama wetu tuwapo majini" Alisema Samwel.
Naye James Mwita ambaye pia ni mvuvi alisema kuwa bei ya vazi okozi ni kubwa hivyo baadhi yao hawamudu kununua kutokana na ukata wa fedha na kuiomba serikali kupunguza bei ili waweze kununua.
Mkurugenzi wa TMFD Bwana Edwin Soko ameiomba Serikali kuitazama sekta ya uvuzi katika jicho la usalama wa wavuvi na kuona namna ya kuweka ruzuku kwenye vifaa vya usalama kama vazi la okozi ili wavuvu wengi waweze kumudu kununua.
"Kwa sasa sekta ya uvuvi inakua kwa kasi hivyo ni vyema ukuaji huu uendane na kasi ya usalama wa shughuli za majini ili kuzuia maafa" Alisema Soko.