TGNP, INTERNEWS ZATOA MAFUNZO UANDISHI WENYE MRENGO WA KIJINSIA KWA WANAFUNZI CHUO KIKUU CHA TUMAINI DAR

MTANDAO wa jinsia Tanzania (TGNP) wakishirikiana na Internews kupitia Mradi wa Boresha Habari wametoa mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia hususani katika kuhamaisha wanawake kushika nafasi za uongozi kwa Wanafunzi wanaosoma Masomo ya Uandishi wa habari katika Chuo Kikuu Cha Tumaini cha jijini Dar es Salaam ili wawe na jicho la kijinsia wakati wa kuandika habari.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2023, Mwezeshaji kutoka Idara ya Mafunzo na Ujengaji Uwezo wa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai, amesema kuwa mafunzo hayo pia yatawajengea uwezo wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika maeneo ya kijamii na tasnia ya habari.

Amesema nchi ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kiitifaki ya kimataifa, Kikanda na kitaifa katika kuufikia usawa wa kijinsia.


Kwa Upande wa Tanzania dira ya Maendeleo ya 2025 inazungumzia kuondoa ubaguzi, utofauti wa rangi na jinsia katika kushiriki masuala ya shughuli za kiuchumi lakini pia inazungumzia jamii ya kitanzania wenye usawa na uwezo katika masuala yote ya kiuchumi, kijamii na masuala ya kisiasa na kiutamaduni.


Akizungumzia umuhimu wa Waandishi wajao kuwa na mafunzo hayo Anna amesema kuwa wanatakiwa kuelewa kwa ufasaha masuala ya kijinsia, uhalali wa kuzungumzia masuala ya kijinsia pia waweze kuandika taarifa ambazo zitabadilisha jamii na kuwa na mtazamo chanya kwenye masuala ya kijinsia na kuongeza ufanisi katika maendeleo kwenye makundi yote.


"Makundi yote yakiwa katika hali ya usawa wa kupata fursa, kushiriki katika masuala ya maendeleo na kupata taarifa na elimu, inamaana hata maendeleo ya nchi yatakuwa yanaenda haraka kwasababu watu wengi watakuwa wanashiriki", ameeleza Anna.


Kwa upande wa Mratibu wa mafunzo wa Mradi wa Boresha Habari kutoka Internews, Mariam Oushoudada amesema mafunzo hayo yataenda kusaidia wanafunzi katika kuhakikisha kunakuwa na uwiano wa uongozi katika tasnia ya habari.


"Uwiano huo ni kuanzia Vyuoni mwao hadi watakapomaliza masomo yao. Mafunzo haya yatakuwa endelevu ili waweze kuandika habari ambazo zitakuwa na usawa wa kijinsia bila kukandamiza jinsi yeyote katika jamii",ameeleza.


"Mafunzo haya yamekuja baada ya kuona Viongozi mbalimbali hawaandikwi vizuri kwenye habari, hivyo tukitoa wanahabari wenye mafunzo ya kijinsia kutoka vyuoni kutakuwa na uwiano sawa katika namna ya kuandika habari zitakazoleta maendeleo na kukua uchumi wa nchi",amesema.


Kwa upande wa Mohamed Karim amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kukuza uelewa pale wanapoandika habari katika jamii kwa kuzingatia ujinsia.


"Jamii itabadilisha fikra zao bila kupendelea jinsi moja na kuikandamiza jinsia nyingine pia kutokukandamiza makundi maalumu mengine.


Akizungumzia namna alivyonufaika na mafunzo hayo, Mwanachuo kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, Eva Paul amesema kuwa wanajengewa ujasiri wanahabari watarajiwa kuangalia usawa wakati wa kuandika habari katika jamii.
Mwezeshaji kutoka Idara ya Mafunzo na Ujengaji Uwezo wa Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Anna Sangai akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 18, 2023 wakati wa kufungua mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia kwa Wanafunzi katika Kikuu cha Tumaini wanaosoma masomo ya uandishi wa habari. Mafunzo hayo yameandaliwa na TGNP na Internews kupitia mradi wa Boresha Habari.
Mratibu wa mafunzo wa Mradi wa Boresha Habari kutoka 'Internews', Mariam Oushoudada akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 18, 2023 na Wanachuo Kikuu cha Tumaini wanaosoma masomo ya uandishi wa habari  wakati wa mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP na Internews kupitia mradi wa Boresha Habari.
Mhasibu Msaidizi kutoka Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Fauster Sekuba akizungumza na Wanachuo Kikuu cha Tumaini wanaosoma masomo ya uandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 18, 2023 wakati wa mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP na Internews kupitia mradi wa Boresha Habari.
Mtoa Mada Deogratius Koyanga akizungumza na Wanachuo Kikuu cha Tumaini wanaosoma masomo ya uandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 18, 2023 mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP na Internews kupitia mradi wa Boresha Habari.
Wanachuo Kikuu cha Tumaini wakisikiliza mada wakati wa mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia yaliyotolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam Machi 18, 2023.

Wanachuo Kikuu cha Tumaini wanaosoma masomo ya uandishi wa habari wakiwa katika Picha ya pamoja jijini Dar es Salaam Machi 18, 2023 mara baada ya mafunzo ya Uandishi wenye mrengo wa kijinsia yaliyotolewa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania na Internews kupitia Mradi wa Boresha Habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post