Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalage akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22,2023 wakati akitoa tamko kuhusu tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha Mwanafunzi mkoani Mwanza hivi karibuni.Mshauri wa Masuala ya Elimu- HakiElimu, Dkt.Wilberforce Meena akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22,2023 wakati HakiElimu wakitoa tamko kuhusu tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha Mwanafunzi mkoani Mwanza hivi karibuni.Mkuu wa Miradi HakiElimu Bw.Godfrey Boniventura akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 22,2023 wakati HakiElimu wakitoa tamko kuhusu tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha Mwanafunzi mkoani Mwanza hivi karibuni
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
****************
NA EMMANUEL MBATILO, DA ES SALAAM
Shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia masuala ya elimu nchini, Haki Elimu wamependekeza dhana ya adhabu chanya kupewa mkazo katika mafunzo tarajali na kazini kwa walimu ili kuwasaidia kuepukana na matumizi ya adhabu za kikatili.
Mapendekezo hayo wameyatoa leo Machi 22,2023 wakati wakizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutoa tamko kuhusu tukio la adhabu iliyopelekea kifo cha Mwanafunzi mkoani Mwanza hivi karibuni.
Ikumbukwe kuwa tukio hilo la Mwanfunzi Gloria Faustine (14) Kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mwinuko, halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mwanza kufariki ilitokana na kuangukiwa jiwe wakati akichimba kifusi kama sehemu ya utekelezaji wa adhabu aliyopewa pamoja na wenzake kwa kosa la kuzungumza lugha ya Kiswahili katika mazingira ya shule.
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu Dkt. John Kalage amesema walimu wanajukumu la kuwafundisha na kuwajenga wanafunzi katika mwenendo unaofaa na jukumu hili wanaweza kulitekeleza kwa kutumia mbinu mbinu mbalimbali ikiwamo utoaji wa adhabu chanya ambazo zitasaidia kufikia malengo ya utoaji wa adhabu.
"Tunapenda kusisitiza kuwa, adhabu zitolewazo kwa wanafunzi ni lazima zizingatie sana aina ya kosa au tabia inayokusudiwa kurekebishwa, na zilenge katika kumsaidia mtoto kuwa bora zaidi badala ya kumuumiza na kumwongezea hofu". Amesema Dkt.Kalage.
Amesema kuwaadhibu wanafunzi kwasababu za kitaaluma kama vile kushindwa kuzungumza kiingereza, kuandika au kukokotoa kwenye hisabati hakuwezi kutatuliwa kwa kumpa mwanafunzi adhabu ambayo haimwelekezi katika kujifunza kile anachotakiwa.
"Katika mazingira haya, mwalimu angeweza kuagiza wanafunzi waandike insha ya lugha ya Kiingereza, kusoma vitabu vingi vya hadithi za Kiingereza na kutoa tafsiri". Amesema
Pamoja na hayo Hakielimu imetoa rai kwa Serikali kurejea upya mapendekezo yanayotolewa na wadau kuhusu matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia ngazi ya Sekondari.
Dkt.Kilage amesema wanafunzi wanaotoka shule za msingi na hasa za umma kuingia kidato cha kwanza, wanakuwa hawajawa tayari kuweza kutumia lugha ya Kiingereza katika kuzungumza na kujifunzia.
Social Plugin