Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAELEKEZA LUGHA ZA KIINGEREZA NA KISWAHILI KUTUMIKA WAKATI WA UTUNGAJI WA SHERIA .

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro akiwasilisha taarifa inayohusu Muundo na Majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Tarehe 12 Machi, 2023.

Sehemu ya wanakamati wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Viongozi wa Taasisi za wizara hiyo wakifuatilia taarifa ya Mhe. Waziri Ndumbaro.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo (Mbele kushoto) akiandika maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wakifuatia mazungumzo wakati wa kikao cha Wizara ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.

********************

Na George Mwakyembe & Lusajo Mwakabuku – WKS.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeielekeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia lugha zote mbili wakati wa utungaji wa Sheria na kanuni yaani Kiingereza na Kiswahili ili kuepusha kazi hiyo kufanywa mara mbili kunakopelekea kuongezeka kwa gharama rasilimali fedha na muda pale Sheria husika inapotakiwa kutafsiriwa baada ya kupitishwa.

Maelekezo hayo yametolewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria walipokuwa wakipokea taarifa inayohusu Muundo na Majukumu ya Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, 12 Machi, 2023.

Akiwasilisha taarifa mbele ya Kamati hiyo, Waziri Ndumbaro akiwa ameambatana na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zote zilicho chini ya Wizara ya Katiba na Sheria amesema Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha inasimamia ipasavyo suala la haki na usawa jambo linalopelekea wawekezaji kuvutiwa kuwekeza nchini.

"Wizara ya Katiba na Sheria ni Wizara inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kuvutia wawekezaji kwa kuimarisha Haki na Usawa, wawekezaji hawawezi kuja kuwekeza nchini kama hakuna Haki na Usawa”. Alisema Mhe. Ndumbaro.

Akichangia kwenye kikao hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mh. Jaji Dkt Eliezer Feleshi amesema jukumu kubwa lilopo Sasa ni kuendelea kutafsiri Sheria zote 446 pamoja na Sheria ndogo 29,172 na tayari Wizara ilishajipanga na wanaendelea na kazi hiyo, maelezo haya yalipelekea wajumbe kutaka utungaji wa Sheria hizo ufanyike katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili kuepusha kazi ya kutafsiri baada ya mswada wa Sheria kupitishwa.

Pamoja na jukumu hilo Jaji Dkt Feleshi amesema ofisi yake pia ina jukumu la kusimamia majadiliano ya migogoro mbalimbali iliyopo Mahakamani ili migogoro hiyo iijadiliwe nje ya Mahakama kama Kauli Mbiu ya Wiki ya Sheria iliyofanyika February mwaka huu iliyoelekeza umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof, Elisante Ole Gabriel ameishukuru Wizara kwa Ushirikiano wanaowapa na kusema sasa wamejipanga kuboresha Mahakama za Kata nchi mzima kuhakisha kuwa zinakuwa na miundo mbinu bora na ya kisasa.

Katika hatua nyingine, Kamati imeelekeza kuendelea kukiimarisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwani ni moja kati ya vyuo vinavyoipa sifa nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa Chuo bora chenye kuendeleza watumishi wa Mahakama. Kamati vile vile imeelekeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambacho ni chombo cha Kikatiba chenye jukumu la kuhakikisha linalinda haki za binadamu hususani masuala ya makundi maalumu ya wanawake na watoto kutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu na watu yanapojitokeza badala ya kukaa kimya.

Baada ya wasilisho na maelekezo ya kamati, Mhe. Dkt. Ndumbaro alisema kuwa Wizara yake imepokea maelekezo yote na akaiomba kamati kuwa utakapofika wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara na Taasisi zake mbele ya Bunge, kamati iiunge mkono ili bajeti itayoombwa iweze kupitishwa na hivyo kuiwezesha Wizara na Taasisi zake kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com