Katika kuhakikisha wakulima nchini wanalima kwa kutumia zana za kilimo za kisasa na zinakazochochea ufanisi katika uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali ya kilimo na kuwa na hazina ya kutosha ya chakula baada ya mavuno.
Taasisi ya EFTA kwa kushirikiana na Benki ya CRDB pamoja na wazalishaji na wauzaji wa Matrekta ya New Holland kupitia kampuni ya Hughes Agriculture Tanzania wamezindua mafunzo maalumu kwa wakulima, mafunzo yanayolenga kuhimiza matumizi ya zana za kisasa za kilimo, utunzaji wa kumbukumbu na matumizi ya fedha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya kwanza kwa wakulima wa Hanang ambayo yalifanyika katika mji wa Katesh, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi Janeth Mayanja amesema ili wakulima waweze kulima kwa ufanisi ni lazima serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi zishirikiane kutengeneza mazingira Rafiki yatakayo wezesha mkulima kuziona fursa mbele yake.
“Kwa Hanang zipo fursa nyingi sana za kilimo, na hii imechangiwa na uwepo wa ardhi inayokubali karibu mazao yote kwa kila msimu na hivyo kuongeza chachu kwa wakazi wa hapa kujihusisha na Kilimo.”
Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa licha ya ardhi bora kwa kilimo ila upatikanaji wa elimu ya mara kwa mara ihusuyo masuala ya kilimo imekuwa pia ni chachu ya kuwafanya wakulima kulima kilimo bora zaidi.
“Utaona umati huu mkubwa hapa, haujaja tu, wako hapa kuchota maarifa yatakayosaidia kuongeza ufanisi wao shambani”.
Na ndiyo maana kwa niaba ya uongozi wa Mkoa ninawashukuru sana wadau wetu hawa wa EFTA pamoja na washirika wao kwa mafunzo haya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay amesema sambamba na mafunzo juu ya matumizi ya mashine katika kilimo, taasisi yake imewaletea pia wakulima wa Hanang na mkoa wa Manyara kwa ujumla wake, mikopo ya mashine na hasa matrekta ya New Holland ambayo yatakuwa yakipatikana kwa mkopo kwa wakulima bila dhamana.
Bohay ameongeza kuwa kwa sababu wakulima wengi walikuwa hawakopesheki, taasisi EFTA kupitia mkakati wake ilikuja na mpango wa mikopo ambayo haina dhamana ili kutoa fursa nyingi zaidi kwa wakulima kuweza kukopesheka mashine za kilimo.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa licha ya kuondoa kipengele cha dhamana lakini pia wamewarahisishia wakulima namna ya kulipa.
“Wakulima wetu hawa wanategemea kilimo na kilimo siyo shughuli ya kwamba utalima leo na kesho utaanza kuziona hela, Ili mkulima aanze kunufaika na kilimo anahitaji muda ili mazao yakomae mpaka kufikia hatua ya mavuno, na sisi tumeweka utaratibu kuwa marejesho ya mikopo ya wakulima yatakuwa yakifanyika wakati wa mavuno au misimu kwa kipindi cha hadi miaka mitatu ili kutoa nafasi kwa wakulima kupata pesa baada ya kuuza mazao yao ili kufanya malipo” ,amesema Bohay.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wamesema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati na yatawasaidia kuongeza ubunifu katika shughuli zao za kilimo.
“Katesh tunategemea kilimo maana asilimia karibu 90 ya watu wa hapa ni wakulima, changamoto tuliyonayo wengi wetu licha ya kuwa na maeneo makubwa ya kulima bado hatujaweza kuwa na uwezo wa kumiliki mashine nyingi za kilimo kwa wakati mmoja hali inayofanya tusiweze kulima maeneo makubwa, na hii inasababishwa na bei kubwa ya mashine hizi ambazo wakulima wengi hatuwezi kulipa mara moja.
Hata hivyo tunawashukuru sana EFTA maana kupitia wao sasa tunao uhakika tutaweza kumiliki matrekta zaidi na tutaongeza maeneo zaidi ya kilimo na kupata mavuno zaidi.
Sambamba na hilo wakulima hao wameiomba serikali kuendelea kuwasaidia wakulima kutafuta masoko makubwa ya nje ambayo wataweza kuuza mazao yao kwa bei nzuri zaidi
Taasisi ya EFTA inakusudia kutoa mikopo ya matrekta zaidi ya mia 200 kwa wakulima nchi nzima katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu hatua ambayo inaelezwa kuwa itasaidia kuongeza ufanisi kwa wakulima na kulihakikishia taifa akiba ya chakula.
Social Plugin