Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akiangalia shughuli za uzalishajimali za kikundi cha vijana wa St. Vidicom alipofanya ziara halmashauri ya Manyoni kwa lengo la kukagua na kufuatilia uratibu wa utekelezaji wa sera na sheria za uwezeshaji vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na viongozi wa halmashauri ya Manyoni na vijana wakati wa ziara yake kukagua na kufuatilia uratibu wa utekelezaji wa sera na sheria za uwezeshaji vijana na Watu wenye Ulemavu kupitia mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10 na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akikagua kitalu nyumba (Greenhouse) alipotembelea mradi huo katika halmashauri ya Ikungi unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia programu ya kukuza ujuzi.
Mnufaika wa Mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Greenhouse), Bi. Frida Dustan (kushoto) akieleza jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi alipotembelea vijana hao katika halmashauri ya Singida Vijijini – Ilongelo.
Mnufaika wa mafunzo ya stadi za kazi Bw. Harry Stone wa tatu kutoka (kulia) akieleza jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi alipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu – Sabasaba, Mkoani Singida ili kufuatilia utekelezaji wa mafunzo yanayotolewa kwa vijana wenye Ulemavu.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akiangalia nguo iliyoshonwa na vijana wenye Ulemavu fani ya ushonaji alipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu – Sabasaba, Mkoani Singida.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na vijana wenye Ulemavu alipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu – Sabasaba, Mkoani Singida ili kufuatilia utekelezaji wa mafunzo yanayotolewa kwa vijana 108.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
Na Mwandishi Wetu, SINGIDA
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewataka Maafisa Vijana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji katika miradi ya vijana wanufaika wa mikopo yenye riba nafuu inayotolewa na serikali.
Ameeleza kuwa, mfumo huo wa ufuatiliaji utawawezesha kutambua kwa karibu miradi yenye tija ambayo vijana wamewekeza sambamba na kujua hali ya utekelezaji wa shughuli zao za kujikwamua kiuchumi na kuwaletea maendeleo.
Mhe. Katambi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na vijana katika ziara yake ya kikazi mkoani Singida ya kukagua na kufuatilia uratibu wa utekelezaji wa sera na sheria za uwezeshaji vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya Halmashauri ya asilimia 10, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na haki na stahiki za watu wenye ulemavu.
Amesema Serikali kupitia halmashauri zilizopo nchini imekuwa na wajibu wa kutenga fedha kupitia makusanyo ya mapato ya ndani ambapo mikopo ya asilimia nne kwa Vijana, asilimia nne wanawake na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu imekuwa ikitolewa kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha miradi, kuendeleza shughuli zao ambazo zitatoa fursa za ajira na kuwaingizia kipato.
“Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuwezesha vijana kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu ili wajiajiri na kuajiri vijana wenzao kupitia shughuli za kiuchumi watakazoanzisha,” amesema
Aidha, Naibu Waziri Katambi amewataka Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuangalia namna bora ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo hiyo na kuwapatia ujuzi ambao utawasaidia kuanzisha miradi yenye tija, kusimamia shughuli zao sambamba na kuwajengea mbinu za kukuza biashara.
Pia, amehamasisha halmashauri kuwa na utaratibu wa kukopesha tena vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu ambavyo vinarejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Vile vile, amesema katika kuimarisha uwezeshaji wa vijana kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kusimamia na kuhakikisha kila halmashauri inatenga maeneo kwa ajili ya vijana kufanya shughuli zao kiuchumi.
Naye, Mnufaika wa kikundi cha Chapa Kazi, Mwanahamisi ameishukuru serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa kutambua mchango wa vijana katika kusukuma gurudumu la maendeleo, hivyo wameahidi kuchapa kazi kwa bidii na uzalendo ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kuwafanya wananchi wengine waweze kunufaika na fursa hiyo.
Mara baada ya ziara hiyo ya kutembelea vikundi vya vijana vilivyonifaika na mikopo inayotolewa na halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana katika halmashauri ya Manyoni, Ikungi na Singida Mjini, Naibu Waziri Katambi alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu – Sabasaba, Mkoani Singida na kujionea utekelezaji wa mafunzo yanayotolewa kwa vijana 108 wenye Ulemavu. Pia alitembelea vijana wanufaika wa mafunzo ya kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Greenhouse) katika halmashauri ya Ikungi na Ilongelo, Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia programu ya kukuza ujuzi.