Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga akizungumza na Waandishi wa habari Dodoma.
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA
KUTOKANA na maboresho yanayoendelea kufanyika kwenye Mfuko wa Taifa wa bima ya afya nchini (NHIF), Mfuko huo umewatoa hofu wanachama wake kufuatia taharuki iliyojitokeza kuhusu Mfuko huo kutangaza kuondoa fao la "Toto Afya Kadi".
Akiongea na wananchi kupitia vyombo vya habari Jijini hapa, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga amesema hali hiyo haiwezi kuathiri huduma za afya na kwamba hayo ni maboresho ya utaratibu wa usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa bima hiyo.
Amesema kutokana na maboresho hayo, kwa sasa wazazi na walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao kwenye bima ya afya au kuwasajili kupitia shule wanazosoma Ili kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote.
Amefafanua kuwa wanachama katika makundi hayo watatakiwa kujiunga kama familia au kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule wanazosoma.
"Mpango wa Toto Afya Kadi ulianza rasmi 2016 baada ya kufanyiwa upembuzi lengo likiwa ni kuwajumuisha watoto kupitia shule zao,nia yetu ni kuwafikia kundi kubwa la watoto chini ya miaka 18 ambao takwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi wote na kufikia azma ya Serikali ya watu wote kuwa na bima ya afya,"amesema.
Pamoja na hayo amesema uzoefu wa miaka saba wa kulihudumia kundi hilo la watoto kupitia Toto Afya Kadi umewezesha Mfuko huo kufikia watoto 210,664 walio chini ya miaka 18 na kupelekea Mfuko kujifunza mengi yanayohitaji kufanyiwa kazi na kuyaboresha.
"Kati ya hayo ni pamoja na usajili wa mtoto mmoja ambayo inachelewesha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya ambayo inataka watu kujiunga kwa wingi,aidha NHIF umeendelea kushirikiana na shule za msingi na Sekondari ili kusajili wanafunzi na mwitikio unaonekana,tunaamini hii ndo njia sahihi ya kuendelea nayo Ili kuhakikisha watoto wengi wanufaika,"amesisitiza
Amesema, maboresho ya utaratibu wa usajili wa hiari kwa kundi hilo la watoto walio chini ya miaka 18 mzazi au mlezi anashauriwa kuandikisha mtoto kama mtegemezi kupitia bima zao kwa mwajiri au vifurushi vya Najali afya,wekeza afya na Timiza afya pamoja na wazazi wao.
Aidha vifurushi hivyo vinawezesha mtu yeyote mwenye umrí wa zaidi ya miaka 18 kujiunga yeye mwenyewe au na mwenza wake au na watoto wake wasiozidi wanne Wenye umrí usiozidi miaka 18 na wanufaika na huduma za matibabu popote nchini kwenye vituo vilivyosajiliwa na NHIF.
"Kundi la watoto watakao Kosa sifa na vigezo vya kuandikishwa kupitia bima ya afya ya wazazi kwa mwajiri au vifurushi vya Najali afya, wekeza afya na Timiza afya wanaweza kuandikishwa kupitia vyuo , shule au vituo rasmi vya kulelea watoto waishio katika mazingira magumu,"anafafanua
Kwa watoto walio chini ya miaka mitano Mkurugenzi huyo amefanua kwamba ambao watashindwa kuandikishwa kupitia machaguo hayo wanapaswa kutumia fursa ya matibabu bila malipo katika vituo vya Umma kama ilivyoainishwa kwenye sera ya afya ya mwaka 2007.
Akieleza faida za usajili wa watoto kupitia shule zao ni pamoja na kuwezesha utekelezaji wa dhana ya bima ya afya kwa wote utaratibu utakaowapa nafuu wazazi kugharamia matibabu ya watoto wao na kuwa na uhakika wa matibabu ikiwa ni pamoja na kuwajenga watoto dhana ya bima ya afya tangu wakiwa wadogo.
"Manufaa ya kusajili watoto kupitia kaya au familia ni kuwezesha familia nzima kunufaika na si mtoto tu au baadhi ya watoto tu utaratibu huu pia utawezesha wazazi kupanga mipango ya kugharamia nafuu wa afya na hivyo kuepuka umaskini usio wa lazima,"amesema.
Aidha Mkurugenzi huyo wa NHIF ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo umeanza juzi Machi 13,2023 na Mfuko ulitoa taarifa rasmi Kwa Umma na kwamba Mfuko Katika Ofisi zake zote upo tayari kuelimisha na kutoa ufafanuzi Kwa wote wanaohitaji kufahamu zaidi.
Kutokana na hayo jamii inapaswa kuelewa kuwa vifurushi vya bima ya afya ni mpango unawezesha mwananchi mmoja mmoja au familia kuchagua na kuchangia huduma za matibabu kabla ya kuugua na Kisha kuwa na uhakika wa matibabu kwa kutumia Kadi ya bima ya afya bila kikwazo cha pesa.
Social Plugin