RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUWEZESHA WATU WENYE ULEMAVU



Na Mwandishi Wetu, TANGA

Kamati ya kudumu ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii imempongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Fatuma Toufiq ameyasema hayo Machi 15, mwaka huu wakati kamati ilipotembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye ulemavu cha Masiwani kilichopo jijini Tanga.

Mhe. Toufiq amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia imehakikisha hakuna mwenye ulemavu ambaye ameachwa nyuma bila kupewa ujuzi mbadala wa kujikwamua kimaisha na imekuwa ikigharamia huduma zote.

Aidha, ametoa rai kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako kuweka utaratibu wa kuwapatia zabuni za kazi watu wenye ulemavu ikiwamo za chuo hicho ili kuonesha umahiri wao.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameitaka jamii kuacha kuwafichua watu wenye ulemavu ili wawezeshwe na kupata haki zao za msingi ikiwemo kusikilizwa, kupata ujuzi na kuendelezwa kielimu.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema maelekezo ya Rais Samia ni kuimarisha huduma za utambuzi wa mapema na afua za utengamao kwa watu wenye ulemavu ambao hadi sasa kwa Mkoa wa Tanga watoto 297 wametambuliwa.

Amesema licha ya Rais Samia kutoa fedha kwa vijana kwa ajili ya kupata ujuzi ikiwamo watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2023/24 zimetengwa sh. bilioni tatu kwa ajili ya kuendeleza vyuo vitatu vya watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Ruvuma, Songwe na Kigoma.

Mhe. Prof. Ndalichako ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Ofisi yake itafanyia kazi maagizo waliyoyatoa ikiwemo serikali kuangalia namna ya kuwawezesha kifedha mara baada ya kumaliza masomo yao ili wajikwamue kiuchumi kupitia ujuzi waliopata.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post