Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SDF TUMAINI JIPYA KWA VIJANA KUTOKA MAKUNDI MAALUM NA WENYE ULEMAVU


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Huenda kiu ya watu wenye ulemavu kupata elimu juu ya vile wanavyovipenda ikawa imepata majibu baada ya Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kuja na programu inayowawezesha kupata ujuzi katika vyuo mbalimbali vya Ufundi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia (WB) ambayo yamekuwa yakiwanufaisha vijana wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali kupata nafasi ya kusoma na kuendeleza ujuzi wao na baadae kuweza kuutumia kujitafutia kipato na kuachana na utegemezi

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye alikaririwa akisema, TEA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekamilisha taarifa ya ufuatiliaji wa wanufaika (Tracer Study) kwa lengo la kupima matokeo ya mafunzo ya kuendeleza ujuzi kwa wanufaika waliopata nafasi kushiriki mafunzo hayo.

Na ufuatiliaji huo ulihusisha wanufaika 3,871 kati ya wanufaika zaidi ya elfu 35,000, ulionyesha kuwa asilimia 81 ya wanufaika hao wameajiriwa au wamejiajiri ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu walipopata mafunzo ya ujuzi ambapo kiasi cha Sh. Bil 13. 8 zimeishatumika ikiwa ni fedha zilizoelekezwa moja kwa moja kwa Taasisi 143 za Mafunzo ili kuwezesha mafunzo.

Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho Yombo kwa watu wenye Ulemavu ni moja ya Vyuo vinavyotoa mafunzo kwa wanufaika wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), ambapo vijana wenye ulemavu takribani 93 wanaendelea kupatiwa mafunzo ya Ujuzi katika fani mbalimbali ili waweze kuwa na ujuzi ambao utawasaidia kujipatia kipato.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho Yombo kwa watu wenye Ulemavu Bi.Maria Chilambo ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ufadhili walioupata kwani walitengewa zaidi ya milioni 118 kwa ajili ya kutoa elimu ya mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 120.

Amesema, Fedha walizozipata zililenga kufundisha fani nane ambazo ni fani ya useremala, uokaji keki na mikate, uchomeleaji, umeme wa majumbani, ushonaji wa nguo, urembo, utengenezaji wa batiki pamoja na fani ya kilimo.

Aidha amesema, vijana 93 wamepata mafunzo hayo kati ya vijana 120 ambo walilengwa kunufaika kupitia mpango huo wa TEA. Alitoa rai kwa vijana kutoka makundi maalum na wenye ulemavu kujitokeza na kuchangamkia fursa zinapotangazwa ili waweze kujikwamua kimaisha

Hata hivyo amesema tutegemee kupata vijana walioiva kwa mafunzo waliyopewa chuoni hapo na hivyo kwenda kulitumikia vizuri taifa na kutarajia kupata vijana wenye kipato kuondokana na hali tegemezi walizokuwa nazo awali kwani wataenda kujiendeleza na kujiingizia kipato na kuishi maisha ya kujitegemea.

"Tutegmee kuanzisha vitu vipya kwenye maeneo tofauti tofauti kutoka kwa vijana wenye weledi kwasababu kwa miezi hii miwili na mitatu wana kitu walichotoka nacho kwahiyo wataenda kufanya shughuli zao kwa utaalamu zaidi kuliko hapo nyuma ambapo walikuwa wanafanya". Amesema

Amesema usalama wa vijana wanufaika umezingatiwa kwani wamekuwa wakifundishwa kwanza suala la usalama hasa usalama wao binafsi na mahala pa kazi kwa ajili ya kujilinda wao wenyewe, kuwalinda wengine lakini pia kulinda na zile mali ambazo wanazitumia kwa masilahi ya kwao.

Ameeleza kuwa wameshirikiana na wadau mbalimbali hasa Jeshi la Zima Moto Mkoa wa Temeke ili kuja kutoa mafunzo yanayohusiana na majanga ya moto na vitu vingine vinavyohusiana na usalama wakiwa katika maeneo ya kazi au sehemu wanazoishi kwani wamekuwa wakiwahamasisha vijana kuwa na nyezo za kuzuia hatari yoyote.

Vilevile amesema waliwasisitizia wanufaika kuchagua zile fani ambazo kulingana na ulemavu wao pia mtu anaweza akaifanya na isimuhatarishie maisha yake, kwasababu uhai wa mtu ndo waliupa kipaumbele. Na wanashukuru mradi uliruhusu wakabadilisha fani baada ya kufika chuoni.

Mratibu wa Mafunzo katika Chuo hicho ambaye pia ni Mkufunzi wa Fani yaUmeme Bi.Regina Makota amesema Mafunzo yamekuwa na manufaa makubwa kwa vijana kwasababu wameweza kuwaibua vijana wenye ulemavu kutoka kwenye mazingira hatarishi hasa kuzingatia wengi wao wametoka mikoani, ni wale vijana ambao walikuwa wanajishughulisha na masuala ya ufundi lakini ule ufahamu wa kuingia darasani walikuwa hawana.

Amesema TEA imejitahidi kwa kiasi kikubwa kujaribu kuingia kwenye halmashauri pamoja na Serikali za Mitaa kuona kuna vijana gani wapo wa aina ya ulemavu ambao wanaweza wakawapa ujuzi na maarifa ambayo wakitoka pale wanaweza kwenda kujiajiri.

Kwa upande wa Wanufaika wa Mradi huo katika Chuo hicho wamesema baada ya kupata mafunzo hayo wanategemea kwenda kuyatumia mafunzo hayo kwa kujiajiri na kuweza kujipatia kipato cha kuweza kujikimu na kuachana na hali ya utegemezi.

Nae Mwanafunzi wa Fani ya useremala Bw.Bahati Abdallah ambaye ni mlemavu wa kuongea na kusikia akizungumza kupitia alama ya ishara ameipongeza Serikali pamoja na wadau ambao wamewawezesha kupata mafunzo hayo kwani hadi sasa anamatumaini makubwa ya kuweza kujiendeleza katika kujitafutia ajira kupitia ujuzi ambao ameupata.

Hata hivyo wameiomba Serikali kuwaangalia upya kwenye suala la mitaji kwani wengi wao wamekuwa wakipata fursa ya mafunzo hayo lakini wakihitimu wanashindwa kujiendeleza kutokana na ukosefu wa mitaji ambayo ingeweza kuwasaidia katika kujikimu kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com