WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama,akizungumza wakati akifungua Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma lililofanyika leo Machi 24,2023 jijini Dodoma.
KAMISHNA wa Maadili Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi ,akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma lililofanyika leo Machi 24,2023 jijini Dodoma.
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma lililofanyika leo Machi 24,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama,ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza baadhi ya viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na mgongano wa maslahi nchini.
Agizo hilo amelitoa leo Machi 24,2023 jijini Dodoma wakati akifungua Baraza la wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Waziri Mhagama amesema kuwa wapo baadhi ya viongozi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya mgongano wa maslahi wanapotimiza majukumu yao na wengine kukinza hasa katika halmashauri ambako serikali imeelekeza fedha nyingi za miradi.
“Kwa kutumia mbinu za uchunguzi mlizonazo, fuatilieni kwa ukaribu viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa na mgongano wa maslahi ili haki iweze kutendeka ikiwemno kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika.
”kiongozi wa umma anapotoa kauli inayokinzana na kiongozi mwenzake au na mamlaka iliyomteua ni ukiukwaji wa maadili na tabia hiyo sio nzuri katika kuwaletea wananchi maendeleo.''amesema Mhagama
Hata hivyo amewataka kutumia baraza hilo kukumbushana kuwa wanapotoa elimu kwa viongozi wa umma wakumbushe matumizi sahihi ya madaraka kwa kutunza siri.
“Zingatieni viapo vyenu vya usiri wa taarifa mnazozipata ili na nyie mthaminiwe na muaminike na wadau wenu wa nje na ndani. Kumbukeni kuwa kila taarifa ya kiongozi inayokujia ni siri, isipotunzwa vizuri inaweza kuharibu taswira nzuri ya kiongozi na Serikali kwa ujumla,”amesisitiza
Kwa upande wake Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi amesema watajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 na pia kujadili mipango na mikakati kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa 2023/24.
“Tunaahidi tutaendelea kutekeleza majukumu yetu tuliyokabidhiwa kisheria bila kupoteza uelekeo ili kufikia dira ya kuwa taasisi yenye ufanisi na kuaminika katika kukuza na kusimamia misingi ya maadili ya viongozi wa umm.'amesema Jaji Mstaafu Mwangesi
Social Plugin