Na Dotto Kwilasa, DODOMA
SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii hususan Twitter na Instagram kuhusu malalamiko ya vijana waliokuwa wanafanya shughuli za mafunzo kazi kwa vitendo katika shirika hilo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 10,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Mkeyenge, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Vijana hao.
Mkeyenge amesema kuwa katika malalamiko hayo yanasema Mikataba ya mafunzo kazi kwa vijana zaidi ya 400 waliokuwa TASAC ilivunjwa bila kufuata utaratibu na ikiwa imebaki muda wa mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.
Aidha amesema Vijana hao walifanya kazi bila bima ya afya na kwamba TASAC ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke.
Mkeyenge amefafanua kuwa mnamo mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC.
“TASAC ilikuwa ikitekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokua wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo ya kazi lakini kufuatia mabadiliko hayo, Agosti 11, 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii,”amesisitiza
“Vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi,”amesema.
Mkeyenge ameendelea kufafanua kuwa kwa mujibu wa masharti ya mikataba, TASAC ilikuwa inawapa mkataba ya miezi mitatu na kuongeza muda kila ilipoonekana inafaa kutokana na utendaji kazi wa mtu.
Aidha, mikataba ilikuwa imeainisha utaratibu wa namna ya kuvunja mikataba ya mafunzo kazi na ndio utaratibu uliotumika kuvunja mikataba hiyo.
“Kwa kuwa vijana wanaolalamika walikuwa kwenye mafunzo kazi na sio waajiriwa wa moja kwa moja, TASAC kama taasisi nyingine yoyote ya Serikali haina wajibu wa kuwakatia bima ya afya vijana inaowachukua kwa mafunzo kazi kwani stahiki zao zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazi uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu,
“Ninapenda kuwafahamisha kuwa, TASAC ni taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hivyo basi mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na shauri hili,”amefafanua Mkeyenge
Hata hivyo Mkeyenge amewahakikishia vijana hao kuwa TASAC haijatoa na haiwezi kutoa rushwa yoyote kwa CMA ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.
“Ningependa mfahamu ya kuwa, kati ya vijana 209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41 tu ambao hawakuridhika na maamuzi hayo. Vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 tu ambao shauri lao dhidi ya TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi,
“Lakini Vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa ni nje ya uwezo wa Shirika,”ameeleza.
Amesema kwa kuwa suala hili lipo kwenye chombo cha maamuzi kisheria, TASAC haipaswi kulizungumzia shauri hilo lakini ilionekana ni busara kulitolea ufafanuzi wa kilichofanyika kwa upande wa TASAC na kuacha hatua za maamuzi zinazoendelea kuchukua mkondo wake.
Social Plugin