TBS YAWATAKA WADAU KUSHIRIKI KATIKA UANDAAJI VIWANGO

Meneja wa uandaaji Viwango TBS, Mhandisi Yona Afrika akizungumza na waandishi wa habari hapo jana Machi 20,2023 katika Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam

Afisa Viwango TBS, Mhandisi Prosper Godfrey akizungumza na waandishi wa habari hapo jana Machi 20,2023 katika Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam

*************************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

KATIKA kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Viwango Barani Afrika, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka Wadau mbalimbali kushiriki katika uandaaji Viwango ili kuweza kujijengea uelewa mkubwa kwenye masuala ya uzalishaji na uandaaji wa bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana Machi 20,2023 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa uandaaji Viwango TBS, Mhandisi Yona Afrika amesema maadhimisho hayo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Kanda ya nyanda za juu Kusini Mbeya Machi 27 hadi 28,2023 ambapo wadau wote wanakaribishwa kushiriki.

Aidha amesema kuwa kwa mwaka huu wanataka kuangalia kazi ya uandaaji viwango inavyoweza kuwakuza wajasiriamali wadogo hasa wa kilimo kwenye suala zima la ushiriki katika uandaaji waa viwango.

Kwa upande wake Afisa Viwango TBS, Mhandisi Prosper Godfrey amesema katika maadhimisho hayo Machi 27 kutakuwa na mafunzo kwa wadau mbalimbali wanaojihusisha mazao ya vyakula ikiwemo mchele, matunda na mbogamboga ambapo pia maadhimisho hayo yataendana na utoaji zawadi na tuzo kwa washindi waliopatikana kwenye shindano la Insha.

Amesema TBS ilipokea zaidi ya Insha 250 ambazo zilishindanishwa na kupata washindi 10 ambao watapewa zawadi Machi 28 siku ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Viwango barani Afrika.

"Insha hizi huwa zinafanyika kwa lengo la kukuza uelewa kwa wanafunzi ambao tunatarajia watakao kuja kuwa wazalishaji na watumiaji wa bidhaa wa kesho kwani wanaoandika wanaongeza uelewa juu ya viwango na pia kupitia wao tutazidi kuelimisha jamii juu ya suala zima la umuhimu wa viwango ". Amesema Mhandisi Godfrey.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم