Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEA KWA KUSHIRIKIANA NA TAHA YAFIKISHA KILIMO CHA BUSTANI KWA VIJANA 400

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bi. Bahati Geuzye (Kulia) akisisitiza jambo alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa TAHA Bi. Jacqueline Mkindi (wa pili kushoto) ofisini kwake Jijini Arusha. Kulia kwake ni Mratibu wa Mafunzo wa TAHA Bi. Loveness Adolf na kushoto ni Meneja miradi kutoka TEA Bw. Masozi Nyirenda
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Bi. Bahati Geuzye akiwa ameongozana na Bw. Lugano Ipyana mnufaika wa mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi wakielekea kwenye mashamba anayolima mnufaika huyo kukagua. Wengine ni Masozi Nyirenda Meneja Miradi –TEA (Kushoto) na Simon Mlay Msaidizi Mkuu wa Mkurugenzi – TAHA (Kulia)

Bahati Geuzye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) akiangalia matunda aina ya Karela (Bitter Gourd) yanayolimwa na mnufaika wa Mafunzo ya Ujuzi Lugano Ipyana, aliyepata mafunzo hayo kupitia Taasisi ya TAHA ya Jijini Arusha

Mnufaika wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi Irene Mollel akimuelezea Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye jinsi alivyonufaika na mafunzo hayo yaliyotolewa na Taasisi ya TAHA Jijini Arusha. Kushoto ni Masozi Nyirenda, Meneja Miradi kutoka TEA

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye (wa tatu kulia) pamoja na wataalam wa kilimo kutoka TAHA wakikagua mmea wa nyanya kwenye shamba la mnufaika wa Mafunzo ya Ujuzi Jijini Arusha.

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania Bahati Geuzye (wa pili kulia) kwenye picha ya pamoja na mnufaika wa Mafunzo ya Ujuzi na wataalam wa kilimo kutoka TAHA Jijini Arusha.

**********************

Na Mwandishi Wetu

Matokeo ya Sensa ya watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 nchini Tanzania yalibainisha kuwa, asilimia 34.5 ya watanzania wote ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa. Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha vijana wanahusishwa kikamilifu katika miradi na programu za maendeleo kupitia mafunzo ya ujuzi na Ufundi stadi ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana katika ngazi zote.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika kuunga mkono jitihada hizo za Serikali, ilitoa ruzuku kwa ajili ya Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi katika sekta ya Kilimo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), kwa Taasisi inayojihusisha na Kilimo-Biashara cha Bustani na Mbogamboga (TAHA) mwaka 2021 kwa lengo la kunufaisha vijana 400 kwa kuwajengea uwezo kuhusu kilimo cha bustani (horticulture).

Kupitia ruzuku hiyo ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), jumla ya vijana 437 wamenufaika na mafunzo hayo ambayo yalifanyika katika maeneo mbalimbali ya Jijini Arusha yakitolewa na Taasisi ya TAHA na hadi sasa asilimia 90 ya vijana hao ni wakulima wakubwa wa mbogamboga na matunda wanaofurahia soko la ndani na nje ya Tanzania.

Gilliad Daniel Kiongozi wa Uzalishaji (Production Lead) kutoka TAHA anasema, ruzuku waliyopewa kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) imeleta mabadiliko chanya ndani ya Taasisi yao kupitia programu ya kuendesha mafunzo ya kuwajengea vijana uwezo katika Kilimo cha Bustani baada ya muitikio kuwa mkubwa tofauti na walivyotarajia.

‘‘Makubaliano ya mradi yalikuwa ni kuwafikia vijana 400 hadi unakamilika kwa maana ya kutoa mafunzo ila tulishangaa vijana walivyochangamkia fursa hiyo, mwisho tukafundisha 37 zaidi na hivyo kuwa na idadi ya wanufaika 437, alisema Gilliad’’

Aidha, TEA ilitoa ruzuku kwa Taasisi ya TAHA kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) kwa lengo la kufadhili mafunzo ya ujuzi kwa vijana katika Sekta ya Kilimo kama moja ya sekta za kipaombele ikizingatia kuwa, sekta hii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania. Takwimu na machapisho mbalimbali yamekuwa yakionyesha kuwa asilimia 90 ya ardhi ya Tanzania hulimwa na wakulima wadogo na sekta ya kilimo inatoa ajira kwa asilimia 65.5 na inachangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa, asilimia 30 ya soko la nje na asilimia 65 ya malighafi za viwandani

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi. Bahati Geuzye alifanya ziara ya kikazi Jijini Arusha mwanzoni mwa wiki kwa lengo la kukutana na uongozi wa TAHA lakini pia kuwatembelea baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo ya ujuzi kuona maendeleo yao baada ya kujengewa uwezo kupitia ruzuku ya Mfuko wa SDF

Katika ziara hiyo, Geuzye alifurahia kuona wanufaika wanaendeleza kilimo kwa kutumia utaalam walioupata chini ya TAHA lakini pia alifarijika kusikia kwamba kwao soko siyo changamoto tena maana mafunzo waliyopatiwa yanawasaidia kuzalisha bidhaa zenye ubora kulingana na mahitaji ya soko.

‘‘Nafarijika sana kuona hamkurudi nyuma baada ya mafunzo maana vijana wengi hawapendi kazi za kilimo kutokana na changamoto mbalimbali. Ni wakati muafaka sasa vijana wengine wajifunze kuthubutu na kutokukata tamaa kupitia kwenu mliofanikiwa katika sekta hii, alisema Geuzye’’

Geuzye aliongeza kwamba, Serikali inatambua mchango wa vijana katika kukuza uchumi wa nchi lakini pia mchango wa sekta ya kilimo katika kukuza pato la Taifa. Ndiyo maana vijana wanahamasishwa kuwekeza kwenye sekta hii, kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, wadau na Sekta binafsi kwani kilimo ni muhimili wa maendeleo kwa nchi yetu.

Lugano Ipyana mmoja wa wanufaika alithibitisha hayo kwanza kwa kuishukuru Serikali kwa kuwathamini vijana kisha akasema, yeye alisoma hadi ngazi ya stashahada na kufanikiwa kufanya kazi na makampuni mbalimbali ya watu binafsi ila hakuridhika na kipato alichokuwa akipata kazini kwake hivyo aliamua kutafuta kitu kingine cha ziada cha kumuongezea kipato.

Ipyana anafafanua kwamba, mwaka 2021 alisikia tangazo la kuwezesha vijana kuwajengea uwezo kufanya kilimo cha bustani lililotolewa na TAHA na bila kusita alituma maombi akafanikiwa kuchaguliwa. Mafunzo yalikuwa ya muda mfupi na walijikita zaidi kwenye mafunzo kwa vitendo kitu ambacho kilimjengea uwezo wa kujiamini katika kile alichokuwa anakifanya.

Anafafanua kwamba, wakati wa mafunzo alikuwa na shamba lenye ukubwa wa ekari moja na ndilo alilolitumia kama shamba la majaribio kwa kulima nyanya na pilipili hoho. Wataalam wa kilimo cha bustani kutoka TAHA walimfungia miundombinu ya umwagiliaji na wakamuwezesha pembejeo zikiwemo mbegu na madawa na baadae wakamuunganisha na masoko kwa ajili ya kuuza mazao yake.

‘‘Kwa sasa nina zaidi ya ekari 5 ambazo ninaweza kulima aina 5 za mazao kwa wakati mmoja. Pia nashukuru nilikuwa natamani sana kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la nje na nimefanikiwa, mara ya kwanza nililima maharage (French Beans) nikapata tani 2 ambazo niliuza takribani milioni 16, alisema Ipyana’’.

Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na TEA umeleta mabadiliko chanya kwa vijana kupitia mafunzo ya elimu ya ufundi na stadi za kazi. Takribani vijana 35,000,000 wamenufaika na mafunzo hayo katika sekta sita za kipaombele. Sekta hizo ni utalii na huduma za ukarimu, nishati, kilimo biashara, ujenzi, uchukukuzi na TEHAMA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com