TAASISI ya WAJIBU imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari na Asasi za Kiraia (AZAKI) namna ya kufanya uchambuzi wa masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.Akizungumza mbele ya wadau hao wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo ya siku mbili jana Machi 29, 2023,jijini Dodoma Meneja wa Fedha na Utawala wa Taasisi ya WAJIBU, Jackson Mmary ameeleza hatua kwa hatua umuhimu wa kuwa na wadau kutoka maeneo mbalimbali ili kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.
Amefafanua kuwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) ambayo inahusu masuala ya fedha ni nyenzo muhimu ya kufuatilia mipango ya Serikali Kuu ama Serikali za Mitaa na taasisi za kiraia.
“Tumekuwa tukifanya uchambuzi wa ripoti ya CAG peke yetu kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, sasa tumeona kuna umuhimu wa kuwashirikisha wadau. Kwa muelekeo wa WAJIBU tukasema ukitaka kwenda haraka nenda peke yako lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako, kwa hiyo tukaona ni muda muafaka kuanza kwenda na wenzako,” amesema Mmary na kuongeza:
“Miaka iliyopita tulikuwa tunafanya uchambuzi halafu tunawaletea, sasa hivi tunataka kuwaongeza ili sisi na ninyi tufanye uchambuzi kwa pamoja halafu tukitoka hapa twende mbele. Kwa kufanya hivyo tutawezesha kujenga kwa pamoja yale tuliyokuwa tunayachambua na kuwaletea.
Kwa hiyo hivi sasa nanyi mtakuwa na uwezo wa kuchambua, kwa hiyo tutakuwa na nguvu zaidi kwa sababu ya kuhusika sote kwa pamoja. Kingine kitatuongezea mawanda ya uchambuzi kwani tumekuwa tukifanya uchambuzi kama sisi na kama tulikuwa watu 20 hapa leo wapo zaidi ya 40.”
Kutokana na uwezeshaji uliofanywa, kwa sasa amesema kutakuwa na macho mengine 80 zaidi yale yaliyokuwa yanafanya uchambuzi mwanzoni.
“Sisi WAJIBU na ninyi kuanzia leo tukitembea kwa pamoja tutakuwa tumejijengea uwezo, ninyi mtakuwa mmetujengea uwezo na sisi tunawajengea uwezo, kwa hiyo tutaongeza uzoefu na hasa ninyi mnaofanya kazi mikoani katika halmashauri.
Pia kuna mambo ambayo inawezekana tusiyaone namna ambavyo yanaathiri jamii na kila mtu anahoji ndio maana hapa kuna redio za jamii, magazeti ya kitaifa pamoja na kuna asasi za kiraia. Kwa hiyo tukiweka huo mchanganyiko tutaongeza mawanda, uzoefu zaidi katika kufanya uchambuzi wa mambo yanayoathiri jamii,” amesema Mmary.
Meneja wa Fedha na Utawala wa Taasisi ya WAJIBU, Jackson Mmary akizungumza mbele ya Wanahabari na Wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Mafunzo siku mbili yanayoendelea jijini Dodoma yaliyohusu namna ya kufanya uchambuzi wa masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma,lengo mojawapo ikiwa ni kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.
Baadhi ya Wanahabari na Wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri ukumbini humo wakati mafunzo yakiendelea.
Mmoja wa Wandishi wa habari akichangia jambo katika suala zima la kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.
Ofisa Utafiti na Uchambuzi wa Fedha kutoka Taasisi ya WAJIBU Maureen Mboka akieleza jambo mbele ya Wanahabari na Wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini wakati wa ufunguzi wa Mafunzo siku mbili yanayoendelea jijini Dodoma yaliyohusu namna ya kufanya uchambuzi wa masuala ya uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma,lengo mojawapo ikiwa ni kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.
Wakifuatilia baadhi ya vitabu vinavyohusu Ripoti ya uwajibikaji vinavyoandaliwa na Taasisi ya WAJIBU ikiwa ni sehemu ya kujengeana uwezo wa kuchambua ripoti zinazohusu uwajibikaji wa fedha za umma.
Picha mbalimbali wakati wa Majadiliano wa mafunzo hayo yakiendelea
Ofisa Mawasiliano wa Taasisi ya WAJIBU Hassan Kissena akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiibuliwa wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo yaliyowakutanisha Waandishi wa habari pamoja na Wadau wa Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini
Social Plugin