Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIOGUSWA NA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA NKOMELO WAKABIDHIWA NYUMBA ZAO


Yohana Joseph akiwa na mkewe) baada ya kukabidhiwa na mradi wa bomba la mafuta ghafi ( EACOP) Februari 28, 2023 kama fidia baada ya nyumba yake ( nyumba ya udongo) iliyopo katika kijiji cha Nkomelo, Muleba mkoani Kagera kuwa katika orodha ya zile zitakazobomolewa kupisha ujenzi wa bomba hilo. 
Eustadius Protas ( 30) akiwa na mkewe Mikele Savera baada ya kukabidhiwa nyumba yao mpya baada ya ile ya zamani ( juu pichani) kuwa katika mpango za nyumba zitakazobomolewa katika kijiji cha Nkomelo , Muleba mkoani Kagera kupisha ujenzi wa bomba la mafuta. 


Mtendaji Mkuu wa mradi wa EACOP Martin Tiffen akikabidhi mfano wa funguo kwa mmoja wa wanakijiji cha Nkomelo, Muleba mkoani Kagera Felician Tizija baada ya nyumba zao kusubiri kubomolewa kupisha ujenzi wa bomba hilo linalopita katika mikoa 8 likitokea Hoima nchini Uganda mpaka Chongoleani mkoani Tanga 

************ 

Ilikuwa ni furaha na tabasamu kwa wanakijiji 10 wa Nkomelo wilayani Muleba mkoani Kagera baada ya kukabidhiwa nyumba zao mpya zkama sehemu ya fidia kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) linalotarajiwa kuanza ujenzi baadae mwaka huu. 

Nyumba hizo walizokabidhiwa wanakijiji hao zina huduma zote muhimu, ikiwa ni pamoja na majiko na vyoo vya nje, mifumo ya nishati ya jua, matenki kwa ajili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 5,000 kwa kila nyumba na vitu vingine muhimu yakiwemo madirisha ya kisasa ya vioo. 

"Kusema kweli, sikuwahi kufikiria kumiliki nyumba nzuri kama hii maishani mwangu kwa sababu nilikuwa naishi kwenye nyumba ndogo ya udongo, lakini kumiliki nyumba ya kisasa ni jambo ambalo sikuwahi kufikiria hapo awali," alisema. Jovin Bebwa Thadeo mwenye umri wa miaka 67, baba wa watoto 15. 

Dustan Muganyizi, 54, wakati akipokea ufunguo wa nyumba ya familia yake, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na furaha na hakuweza kuizuia furaha yake. 

"Pia tulipokea pesa za fidia ambazo zilibadilisha maisha yetu kabisa kwa kutuwezesha kufanya vitu mbalimbali vya kimaendeleo kama vile kununua pikipiki, mashamba ya ziada, na Ng'ombe," amesema. 

Muganyizi, baba wa familia ya watoto watano ameongeza kuwa kupewa nyumba ni sehemu ya fidia ambayo imeboresha maisha yao. 

Wawakilishi waandamizi mbalimbali kutoka Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), na viongozi wa serikali ya Muleba walihudhuria pia hafla hiyo ya kukabidhi nyumba hizo. 

Mkurugenzi wa Biashara ya Petroli wa TPDC Dk. Wellington Hudson amesema jumla ya nyumba 292 zitajengwa kwa ajili ya watu walioathirika na mradi ambapo kati ya hizo, 58 tayari zimejengwa katika maeneo mbalimbali litakalopita bomba hilo. 

Amesema makabidhiano hayo ya nyumba kwa walioguswa na mradi ni ishara tosha kwamba mchakato wa fidia kwa walioguswa na mradi unaendelea bila vikwazo vyovyote. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EACOP Martin Tiffen , kabla ya kusaini mikataba, wananchi walioguswa na mradi walishirikishwa katika mchakato wa malipo na tathmini kwa ajili ya fidia zao. 

Amesema kuwa watu 9898 walioguswa na mradi ambao ni sawa na asilimia 97 sehemu yao ya mashamba ndio yamepitiwa na mradi . 

Amesema watu 344 ambao ni sawa na asilimia 3 iliyobaki, nyumba zao ndio zimepitiwa na mradi na zitabomolewa kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bomba hilo la mafuta ghafi. 

Bosi huyo wa EACOP aliongeza kuwa 90% ya watu hao ambao nyumba zao zinapitiwa na mradi walifanya uamuzi wa busara wa kuchagua kujengewa nyumba mbadala za zege ambazo zinajengwa na wakandarasi wazawa kwa kutumia ubunifu kutoka Afrika Kusini. 

Aliongeza kuwa nyumba hizo mbadala ziko chini uangalizi (warantii ) kwa mwaka mmoja ambapo wakandarasi watawajibika kurekebisha uharibifu wowote utakaotokea katika kipindi hicho. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Profesa Mark Mwandosya alipongeza hatua ya EACOP kukabidhi nyumba hizo kwa walengwa akisema kuwa hatua hiyo inatoa ujumbe kwa wanaopinga mradi huo kuwa haki za binadamu pia zinazingatiwa katika utekelezaji wake. 

"Tunazingatia matakwa yote ya jumuiya za kimataifa ikiwa ni pamoja na ulinzi wa mazingira na uhifadhi tunapotekeleza mradi huu wa kimkakati wa kitaifa," 

"Tuliahidi katika kutekeleza mradi huu kuwa tutalinda mazingira na kuboresha maisha ya watu wetu kijamii na kiuchumi", alisema Profesa Mwandosya, ambaye alishika nyadhifa tofauti za Uwaziri katika serikali ya awamu ya nne. 

Aziz Mlima, ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda alisema Tanzania iko katika hatua nzuri ya utekelezaji wa mradi huu na kusema kuwa amefurahishwa na hatua iliyofikiwa katika maeneo tofauti ya mradi huo aliyowahi kuyatembelea. 

Ntaki Charles Mayunga, Kaimu Mtendaji wa Wilaya ya Muleba aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya Abel Nyamahanga amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo umekuwa na tija katika kukuza uchumi wa wakazi wa Nkomelo kwa kutengeneza ajira. 

EACOP imepewa leseni ya kujenga miundombinu ya usafirishaji wa mafuta ghafi yenye urefu wa kilomita 1443 ambazo zitasafirisha mafuta ghafi kutoka Kabaale - Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania kwa ajili ya kusafirisha katika soko la kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com