Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MPWAPWA ATANGAZA OPERESHENI KUKAMATA WAIBA VYUMA RELI SGR, NANE WAKAMATWA, WENGINE WAJISALIMISHA


Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Mhe. Sophia Kizigo akizungumza na Wananchi Kata ya Berege, kijiji cha Berege


Na Mwandishi Wetu Michuzi TV -Mpwapwa

MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma Sophia Kizigo amesema kwa sasa wanaendelea na operesheni maalum ya kukamata watu wanaoiba vyuma vilivyofungwa kwenye minara ya kupitisha nyaya za umeme kwenye mradi wa reli ya kisasa ya SGR.

Kwa mujibu wa Kizigo hadi sasa jumla ya watu nane katika Kata ya Berege, kijiji cha Berege ambako mradi wa SGR imepita wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa vyuma hivyo na kisha kuuza kwa wananchi kwenye baadhi ya Wana kijiji.

Akizungumza hivi karibuni Wilayani Mpwapwa, Mkuu wa Wilaya Kizigo amesema katika ujenzi wa reli hiyo TRC na TANESCO ndio wanaohusika na ujenzi kwa maana ya TRC wanajenga miundombinu ya reli hiyo na TANESCO wanaoweka miundombinu ya minara ya kupitisha nyaya za umeme kwa ajili ya treni ya SGR.

"Sasa kilichotokea kwenye ile minara ya kupitisha njia za umeme wahuni wameiba vyuma kwenye minara,wanafungua vyuma wanaenda kuuza tulivyofahamu hivyo ,tulifanya uchunguzi wa kimya kimya ili tuweze kuwashika hao watu na tukakamata baadhi ya watu.

"Mpaka sasa watu nane wamewekwa ndani na tuliwakamataje, kuna watu tuliwakuta kwenye kuta za nyumba zao wamefunga hivyo vyuma, wengine gereji , na wakiulizwa wanasema wameuziwa , unamuuliza aliyemuuzia hivyo hivyo unamfuata unamkata.

"Kuna watu walikuwa wamefungiwa hivyo vyuma na hawavijui ,wenyewe wamelipa tu fedha lakini hata kama ufahamu si umenunua mwisho wa siku tunaweza kushitaki Kijiji kizima. Kwa hiyo ikabidi Aprili 13 mwaka huu tukafanye mkutano na baada ya kufanya mkutano malengo makubwa yalikuwa mawili,"amesema.

Amefafanua lengo la kwanza aliamua kuchukua watu wa TANESCO kutoka mkoani na akawataka kwanza wakatoe elimu kwa wananchi kwamba vile vyuma kwanza vina namba na vimetengenezwa kwa maombi maalum, kwa hiyo havifanani na vyuma vyovyote.

"Kikiibwa kitajulikana tu kipo tofauti, kwa hiyo nilitaka wawape elimu kwanza madhara ya hicho kilichofanyika kwasababu kwenye zile nguzo unapochomoa machuma unafanya kiwe dhaifu inapofika kipindi treni inaanza kazi ikipita tu pale lazima kutokea ajali kwa sababu zile nguzo ndio zimeshika zile nyaya Kwa hiyo ni changamoto kubwa.

"Baada ya kuwapa elimu nikatoa muda kuanzia saa Saba mchana hadi saa 12 jioni wenye hivyo vyuma wavipeleke kwa Ofisa Mtendaji Kata, tuliwapa nafasi ya kwenda kuvisalimisha kwa Mtendaji wa kata na baada ya hapo tutaendelea na operesheni na tutayemkuta na hicho chuma atakuwa amedhamiria.


Kwa hiyo tukawapa hiyo nafasi ,wananchi wakafurahi kwasababu walikuwa hawana amani lakini pia tulifanya hivyo ili watu waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali."



Baadhi ya Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo (hayupo pichani) wakati mkutano ukiendelea







Moja ya Vyuma ambavyo vimekuwa vikiibiwa kwenye mradi huo kikioneshwa kwa Wananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com