Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAFUNGUA TAWI KALIUA, RC BATILDA ASEMA KWELI NI BENKI INAYOMSIKILIZA MTEJA...ULIPO TUPO!


Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Benki ya CRDB imefunguaTawi la Benki ya CRDB Kaliua Mkoani Tabora huku ikiwataka wananchi kuchangamkia fursa za maendeleo zinazotolewa na Benki hiyo.


Akizungumza wakati wa sherehe ya ufunguzi rasmi wa tawi la benki ya CRDB – Kaliua,leo Ijumaa Machi 31,2023, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Buriani ameipongeza Benki ya CRDB kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kufikisha huduma za kibenki kwa wananchi huku akitoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB ikiwamo kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti.

“Ni furaha kubwa kwetu sisi wana Kaliua na Mkoa wa Tabora kwa ujumla kuona Benki yetu ya kizalendo ya CRDB ikiishi kwa vitendo kauli mbiu yake isemayo “Benki inayomsikiliza Mteja” kwa kuyafanyia kazi mahitaji halisi ya wateja wake kwa kuendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja na Watanzania kwa ujumla.

Napongeza sana juhudi hizi kwani hii ni ishara tosha kuwa Benki ya CRDB imejipanga vilivyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha mipango yake ya kujumuisha Watanzania wengi zaidi katika mfumo rasmi wa fedha yaani financial inclusion”,amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Amesema Benki ndicho chombo kikuu cha kutolea huduma za kifedha kwa wananchi na kwamba Benki zinatakiwa zizingatie mahitaji ya wananchi na ziweze kuwahamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kutumia huduma za benki kwa maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla wake.
“Kipekee kabisa niipongeze sana Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha hili. Ni dhahiri kuwa mmekuwa mkiishi kaulimbiu yenu ya “Ulipo Tupo” kwa vitendo kupitia mkakati madhubuti wa kusogeza huduma kwa wananchi, na leo hii mmesogea zaidi hadi hapa kwetu Kaliua, Asanteni sana!”, amesema Dkt. Batilda.


Amezitaja faida za kutumia huduma za benki kuwa ni pamoja na Usalama wa fedha za wateja , Urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya biashara na malengo binafsi na Urahisi wa kufanya malipo kupitia mifumo ya kidijitali.


“Nimefurahi kuona Benki ya CRDB nayo imewekeza katika mifumo hii kwa kiasi kikubwa hii itatusaidia kuongeza wigo kwa wananchi kufanya malipo yao kwa urahisi kupitia SimBanking, SimAccount, Internet banking na CRDB Wakala. Niwapongeze sana kwa hatua kubwa mliyopiga katika eneo hili. Rai yangu kwenu pia ni kuendelea kubuni mipango mbalimbali ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutumia benki. Wananchi waelimishwe kwamba, wakiwa na akaunti benki, pesa zao zinakuwa salama na wakifanya malipo kupitia benki wanajijengea historia nzuri ya kukopesheka”,amesema .

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Kati wa Benki ya CRDB, Erick Willy ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Wakala na Usambazaji wa Huduma mbadala za Kibenki ametoa rai kwa wananchi wa Kaliua na maeneo ya jirani kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB.

Amesema kuwa matarajio ni kuona tawi la Kaliua linakua chachu ya kuchochea shughuli za kiuchumi kwa watu wa Kaliua na maeneo ya jirani na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Tabora ambao ni moja kati ya mikoa yenye historia kubwa katika nchi ya Tanzania.

“Benki ya CRDB ni benki kubwa kabisa ya kizalendo inayoongoza katika amana, rasilimali na mikopo hapa nchini. Benki hii ni moja katika ya matunda ya sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma ambapo mnamo mwaka 1996 Benki ya CRDB ilizaliwa kutoka iliyokuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini”,amesema .

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 27 cha uwepo wake, Benki ya CRDB imefanikiwa kukua na kuongeza mtandao wake wa kutolea huduma kutoka matawi 19 tu mpaka kufikia matawi 240 nchini huku Benki ikiwa pia imetanua huduma zake nchi ya jirani ya Burundi na ipo katika hatua za mwisho kuingia katika soko la DRC.

“Ukuaji huu unaakisi dhima yetu ya kufikisha huduma karibu zaidi na watanzania wote mijini na vijijini lakini pia kutanua wigo wetu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati",ameongeza.
Amesema pamoja na kuwa na idadi kubwa ya matawi 240 yaliyosambaa nchi nzima, Benki yetu pia imekuwa ikibuni na kuingiza sokoni mifumo na njia mbalimbali mbadala zinazorahisisha utoaji huduma kwa Watanzania mfano CRDB Wakala zaidi ya 25,000 nchi nzima, Mashine za kutolea fedha (ATMs) zaidi ya 604, Matawi yanayotembea (Mobile branches 16), Mashine za manunuzi (POS) zaidi ya 1,800, Huduma kupitia simu za mikononi “SimBanking” na “SimAccount” na huduma kupitia mtandao wa internet “Internet banking”.


“Ninajivunia kusema kuwa kupitia mifumo hii ya utoaji huduma, Benki ya CRDB imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa taifa letu na kwa mwananchi mmoja mmoja kwa kuwafungulia milango ya fursa za kiuchumi kupitia huduma na bidhaa zetu, ambazo zimekua zikiongezeka siku hadi siku kulingana na mahitaji ya wateja wetu”,ameeleza.


“Kwa upande wa mkoa wa Tabora, Benki yetu ya CRDB inatoa huduma kupitia matawi 5 na tawi moja kati ya matawi hayo tunalizindua hii leo. Na hivi karibuni tunatarajia kumalizia ujenzi wa tawi jingine lililopo katika wilaya ya Igunga. Lakini pia Benki imekuwa ikitoa huduma kupitia CRDB Wakala, ambapo katika wilaya hii ya kaliua tuna jumla ya CRDB Wakala takribani 48”,ameongeza Willy.


Naye Meneja wa Kanda ya Magharibi, Jumanne Wambura Wagana amesema benki ya CRDB kwa mara ya kwanza ilianza kutoa huduma mkoa mzima wa Tabora kwa tawi moja tu la Tabora lakini baadaye ilipanua wigo kutokana na kupokelewa vizuri na wana Tabora.

Ameeleza kuwa Benki hiyo iliongeza matawi Urambo ,Nzega, na Sikonge huku Kaliua na Igunga wakitumia matawi yanayotembea (Mobile Branches) na kwamba baada ya biashara kukua zaidi na katika kuendeleza mkakati wa kufikisha huduma zake maeneo mbalimbali hususani kwa wananchi na Wajasiriamali ambao hawajafikiwa na huduma za kibenki (unbankable population) benki hiyo imeamua kuweka matawi kamili Kaliua na Igunga mkoani Tabora.


Wagana ametoa shukrani kwa serikali, wafanyabiashara na watanzania wote kwa kuendelea kuitumia CRDB kama benki ya kimkakati katika uwekezaji na kuahidi kuwa wataendelea kuwasikiliza wateja, kuboresha na kuwasogezea huduma watanzania.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Buriani akizungumza wakati wa uzinduzi wa Benki ya CRDB tawi la Kaliua
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Kati wa Benki ya CRDB, Erick Willy ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Wakala na Usambazaji wa Huduma mbadala za Kibenki akizungumza wakati wa uzinduzi wa Benki ya CRDB tawi la Kaliua
Meneja wa Kanda ya Magharibi, Jumanne Wambura Wagana akizungumza wakati wa uzinduzi wa Benki ya CRDB tawi la Kaliua
Mkuu wa wilaya ya Kaliua Dr. Rashid ChuwaChuwa mwenye tai nyekundu pamoja na meza kuu wakiongozana kuelekea eneo la uzinduzi kukata utepe kama ishara ya uzinduzi wa tawi la CRDB Kaliua.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi, Dkt. Batilda Buriani akikata utepe ishara ya uzinduzi rasmi wa Benki ya CRDB tawi la Kaliua
Meneja wa tawi la Kaliua, Fortunatus Masanja akionesha maeneo mbalimbali ndani ya tawi jipya la Kaliua.
Mkurugenzi wa kampuni ya NBS na MNEC wa Tabora akielezea jinsi alivyonufaika na benki ya CRDB na kuwaasa wana Kaliua kuchangamkia fursa CRDB ikiwemo mikopo inayofuata misingi ya dini ya kiislamu Al Barakah,  akaunti mbalimbali pamoja na BIMA.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com