Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamtafuta Mariamu Salumu mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza kwa tuhuma ya kutelekeza watoto wawili kwa kile kinachodaiwa kushindwa kulipa kodi na kusababisha waishi katika mazingira hatarishi huku kijana James Julius akishikiliwa kwa kuishi na watoto hao.
Watoto hao mmoja akiwa na umri wa miaka 17 na mwingine miaka miwili walisafirishwa na mama yao mzazi kwenda Kahama ili yule mkubwa akafanye kazi za ndani na kumlea mdogo wake ambapo walipata msaada kwa kijana Julias aliyedai watakwenda kukaa kwa dada yake na kufanya kazi za ndani ambapo leo imebainika wametelekezwa.
Mama mzazi wa watoto hao alibaki Jijini Mwanza akifanya shughuli za vibarua za mama lishe baada ya kuwasafirisha watoto wake kwa basi hadi Kahama kutokana na ugumu wa maisha.
Tangu watoto hao watoke jijini Mwanza na kwenda Kahama siku 60 zimepita, ambapo baada ya kufika Kahama kijana huyo aliwapatia chumba na kumtaka binti kutafuta kazi za ndani ambapo alifanikiwa kupata na kuamuwa kumuacha mtoto wa miaka miwili ndani pekee yake bila kuwa na uangalizi siku nzima kitendo ambacho kilisababisha mtoto huyo kufanyiwa vitendo vya ukatili vikiwemo vipigo.
Mwenyekiti wa Asasi ya Wanawake Laki Moja Mkoa wa Shinyanga Anascholastica Ndagiwe ambao ndiyo walifanya kazi ya kuibuwa watoto hao amesema baada ya kupata taarifa walifuatulia kwa kushirikiana na dawati la jinsia na kufanikiwa kuwapata huku kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akithibitisha kutokea tukio hilo.
Chanzo - EATV
Social Plugin