Rais William Ruto amemtaja mhubiri Paul Mackenzie kama mhalifu na gaidi kufuatia kufukuliwa kwa maiti kutoka kwa ardhi yake huko Kilifi.
Mchungaji huyo amejikuta katika upande usiofaa wa sheria na upande wa pili baada ya wapelelezi kufichua ibada yake ambayo makumi ya watu wamekufa kwa njaa kwa ahadi kwamba watakutana na Yesu.
Akiongea mjini Kiambu mapema leo, Jumatatu, Aprili, 24 2023 Ruto ambaye alionekana mwenye hasira aliwasuta vikali wachungaji ambao wamekuwa wakitumia imani potofu za kidini kuwapotosha Wakenya.
Alimfananisha Mackenzie na gaidi na kusema anapaswa kufunguliwa mashitaka.
"Kinachoshuhudiwa huko Shakahola ni sawa na ugaidi. Mackenzie ambaye anafanya kazi ya uchungaji kwa kweli ni mhalifu wa kutisha. Magaidi wanatumia dini kuendeleza vitendo vyao viovu. Watu kama Paul Mackenzie wanatumia dini kufanya vitu kama hivi , “Watu kama hawa na magaidi wengine wowote si wa dini yoyote. Wanafaa kuwa gerezani,” Ruto alisema.
Ufukuaji wa miili waingia siku ya nne Shakahola
Rais aligusia suala hilo wakati shughuli ya ufukuaji wa miili ikiingia siku ya nne leo.
Wapelelezi wa Kaunti ya Kilifi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai bado wamekita kambi katika msitu wa Shakahola huko Malindi kutafuta miili ya wafuasi wa mchungaji Paul Mackenzie waliozikwa kwenye makaburi ya halaiki.
Social Plugin