Picha haihusiani na habari hapa chini
Na Mwandishi wetu - Tinde
Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Leticia Daudi Kalegi maarufu 'Mwanandakuna' (62) mkazi wa kitongoji cha Ngaka kijiji cha Nyambui kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye kali shingoni na tumboni na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa mapema jana jioni Aprili 29, 2023 kuna vijana walifika eneo jirani na alipopanga mama huyo wakawa wanavuta sigara lakini wakazi wa eneo hilo hawakuchukulia maanani kwa sababu mtaa ule una mwingiliano wa watu wengi.
“Kuna watu wawili walikuwa jirani chumba cha mama huyu, wakakaa kwa muda mrefu wakivuta sigara na kuchat na simu huyo mama alikuwa anapika chakula cha usiku, wakati mama anatoka kumwaga maji ya kuoshea nyanya/uchafu majira ya saa mbili kasoro usiku ndipo watu hao wakamkaba na kumchoma kwa visu shingoni na tumboni”,wameeleza wananchi kutoka Tinde.
“Huyo mama alikuwa anaishi katika kitongoji hiki hiki na baada ya mgogoro wa ndoa aliondoka kwa mmewe akapanga chumba chake katika kitongoji hiki. Ametoka kwa mme wake miezi kadhaa iliyopita.Tukio hili limetokea wakati kesi ya kugawana mali baina yake na mme wake ipo mahakamani kwani baada ya kuachana na mmewe ambaye yupo Arusha ilifikia hatua ya kugawana mali wiki hii”, taarifa kutoka Tinde zinaeleza.
Inaelezwa kuwa Kesi ya ndoa baina ya mwanamke huyo na mumewe ilikuwa imefikia tamati Alhamis wiki hii Aprili 27,2023 ambapo alipewa talaka kwenye mahakama ya Mwanzo Tinde na kuamuliwa mwanamke apate asilimia 40 na mwanaume asilimia 60 ya mali walizofanikiwa kupata wakiwa kwenye ndoa.
Akizungumza na Mwandishi wetu,i Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngaka bw. Mabula Kuzenza amesema watu waliohusika na mauaji hayo bado hawajafahamika wala chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika.
“Jana Jumamosi Aprili 29,2023 majira ya saa mbili usiku nilipigiwa simu na majirani wa marehemu kwamba kuna tukio kuwa Mwanandakuna ameuawa kwa kuchomwa na visu shingoni na tumboni, baada ya hapo nikapiga simu polisi kwa hatua zaidi”,amesema Kuzenza.
“Waliomchoma visu hawajahamika na chanzo cha mauaji bado hakijafahamika, inaelezwa kuwa kuna watu wasiofahamika walionekana eneo hilo lakini kutokana na kwamba eneo hili limechangamka kuna mwingiliano wa watu hakuna aliyedhani kuna tukio lingetokea… Inasadikika huenda hao ndiyo wamefanya mauaji haya.
Tukio la mauaji limetokea kimya kimya baada ya mama huyo kutoka nje kwenda kumwaga uchafu na ndani ya mtu mfupi majirani wakaona mtu kaanguka chini na kubaini kuwa ameuawa, hata haijulikani imetokeaje tokeaje”,ameeleza Mwenyekiti wa Kitongoji.
Akizungumza na Mwandishi wetu, Diwani wa kata ya Tinde Japhar Kanolo amesema mama huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake alipopanga kitongoji cha Ngaka kijiji cha Nyambui kata ya Tinde kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na tumboni.
“Nilipewa taarifa kuhusu tukio hili la kikatili majira ya saa mbili usiku ambapo wananchi waliokuwa eneo hilo wanasema mapema jana jioni watu waliona vijana wawili wakichat na simu karibu na nyumbani alipopanga mama huyo. Mama huyo alifarakana na mme wake na juzi ndiyo alipata talaka yake mahakamani na kugawana mali walizopata”,ameeleza Kanolo.
Diwani wa viti maalumu tarafa ya Itwangi Mhe. Hellena Daudi Ng’wana mbuli amelaani tukio hilo huku akiomba vyombo vya sheria kuwachukulia hatua kali watu watakaobainika kufanya mauaji hayo ya kikatili.
“Ukatili huu aliofanyiwa mama huyu ni mbaya, wanakosea sana kuua wanawake. Naomba wananchi waache ukatili na vyombo vya sheria vichukue hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na tukio hili”,ameeleza Diwani huyo.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ili azungumzie tukio hilo zinaendelea.
Social Plugin