Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI SHINYANGA KUNYOOSHA KUMBI ZA STAREHE, WAZAZI WANAOHATARISHA USALAMA WA WATOTO SIKUKUU YA PASAKA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 7,2023. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 7,2023. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 7,2023
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 7,2023.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewatahadharisha wazazi na watu wenye kumbi mbalimbali za starehe kwamba Disco Toto na Vibanda Umiza ni marufuku kwa watoto katika kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu ya Pasaka.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Aprili 7,2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema kumbi yoyote itakayokutwa ikichezesha Disco Toto itafungwa katika kipindi chote cha Sikukuu na kufikishwa mahakamani kwa kuhatarisha usalama wa watoto.


“Ni marufuku kwa watoto kwenda Disco toto na vibanda umiza ili kulinda usalama wa watoto. Pia tunawaasa wazazi kutoruhusu watoto wao kwenda kwenye kumbi za starehe kwani kumbi hizo zipo kwa ajili ya watu wazima na siyo watoto. Hivyo tutashughulika pia na wazazi ambao watashindwa kumudu mienendo ya watoto wao katika siku hizi za sikukuu”,amesema Kamanda Magomi.


Kamanda huyo wa Polisi amesema katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu ya pasaka hali ya usalama katika mkoa wa Shinyanga ni shwari kwani tangu kuanza kwa mfungo wa Kwaresma hadi hivi sasa hakuna tukio kubwa lililojitokeza ambalo limehatarisha au kuleta taharuki katika jamii.


“Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawahakikishia wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuwa tutaendelea kuhakikisha kwamba hali hii ya utulivu iliyopo itakuwa ni ya kudumu kwa kipindi chote cha Sikukuu ya Pasaka na hata baada ya Sikukuu”,ameongeza Kamanda Magomi.


“Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawatakia kila la kheri Wakristo wote na WanaShinyanga kwa ujumla katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka. Lakini pia natoa wito kwa madereva wa magari, bodaboda, baiskeli na watembea kwa miguu kuwa makini wawapo barabarani ili kuweza kuepuka ajali zinazoepukika”,amesema Kamanda Magomi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com