Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE HASUNGA AISHAURI SERIKALI TATIZO LA UKOSEFU AJIRA




Mbunge wa Vwawa Japheth Hasunga.


Na Dotto Kwilasa,DODOMA.


KUTOKANA na tatizo la ukosefu wa ajira nchini,Serikali imeombwa kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki yamtu kufanya kazi kwa kuonyesha fursa zilizopo ili kila mtanzania awe na uwezo wa kufanya kazi kujenga uchumi unaoshindana na dunia.


Mbunge wa Vwawa Japhet Hasunga amesema hayo Aprili 10,2023 wakati akitoa mchango wake Bungeni Dodoma kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadilio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024.


Hasunga amesema suala la ajira kwa watanzani bado halijatafutiwa ufumbuzi wa kina na kusababisha maisha ya watanzania Katika maeneo mengi kuwa duni .


Amesema hali ya umaskini iliyopo inatokana na uvivu wa watanzania wengi kuogopa kufaya kazi na kukwepa kuziona fursa zilizopo na kwamba hali hii inarudisha nyuma juhudi za kuingia uchumi wa kati.


"Tatizo la ajira nchini bado ni kubwa, Serikali inapaswa kufahamu kuwa ajira ni haki ya kila mtu na tunaposema ajira iwe ni ajira ya kuajiriwa serikalini na taasisi zake iwe ya kwenye kampuni binafsi ni haki ya kila mtanzania,"amesema.


Akinukuu kifungu cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 11 ndogo ya kwanza , Hasunga amesema mamlaka ya nchi inawajibika kuweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa haki ya mtu kufanya kazi ,haki ya kujipatia elimu na haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee,maradhi au hali ya ulemavu na katika hali nyingine za mtu kuwa hajiwezi.


Amesema bila kuathiri haki hizo mamlaka ya nchi inapaswa kuweka utaratibu wa kuhakikisha kila mtu anaishi kwa jasho lake na hivyo suala la kufanya kazi ni haki ya kikatiba ya kila mtu na kukubali kujielimisha kulingana na stahili ya uwezo wake.


"Serikali ina wajibu wa kumuonesha fursa kila mtanzania afanye kazi na kwa kufanya hivi tutajenga uchumi imara,sote ni mashahidi maisha ya watanzania katika maeneo mengi bado haijaimarika jambo linalopaswa kutiliwa mkazo zaidi,"anasisitiza na kuongeza kuwa;


"Ukiangalia maisha ya watanzania kwa sasa wapo vijana wengi waliosoma katika vyuo vikuu vya kati na wana taaluma mbalimbali na wapo ambao hawajasoma kabisa lakini hao wote ni watanzania ,wote wanatakiwa wapatiwe ajira,na ajira maana yake ni ya kufanya kazi,"amesema Hasunga.


Mbunge huyo Vwawa pia amesema hali bado ni mbaya upande wa mijini na vijijini ambako kuna vijana wengi hawafanyi kazi na kueleza kuwa Taifa haliwezi kujengwa na vijana kutofanya kazi lazima kuwepo na mkakati wa kuhakikisha watu wote wanafanya kazi na pale inapoonekana mtu hana kazi serikali ina wajibu wa kumuonesha fursa ili kila mtanzania afanye kazi kwa bidii.


Akizungumzia ajira Kwa wafanyakazi wa Serikali, amesema bado maslahi yao sio mazuri japo Serikali bado inaendelea kuboresha maslahi yao ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kuleta ufanisi zaidi .


"Lakini wapo wafanyakazi hawa wa sekta binafsi tunawasahu sana wanalipwa viwango vidogo sana haviwawezeshi kuisha maisha ya sasa wala kuwekeza kwa maisha ya baadaye,kwa hali hiyo Tanzania haiwezi kuondokana na umaskini kama nguvu haitaongezwa;


"Naiomba serikali ili watanzania walipe kodi na kujenga uchumi lazima walipwe vizuri na kuongeza ajira,ili kufanikisha hili lazima tuhamasishe ukombozi wa fikra za watanzania ili waone fursa na kujenga uchumi imara,nchi hii ina kila kitu hatustahili kuwa maskini,lazima tukae chini tuone tunatatuaje suala la kuondokana na umaskini,nchi yetu inahitaji zaidi maendeleo ya watu na mtu mmoja mmoja na hapo itakuwa imekombolewa na kuwa ni mahali pazuri pa kufanya kazi ,pa kuishi na kuwekeza,"amesema.


Akizungumzia mchakato wa Serikali kuja na dira mpya ya maendeleo 2025/2050 Hasunga ameiipongeza dira hiyo na kueleza kuwa inalenga kuboresha hali ya maisha ya watanzania.


"Dira hii itawezesha wananchi kuishi maisha Bora,kilichobaki sasa ni kuona kila mtu anafanya kazi na tujuane kupitia kazi zetu na tujue unafanya kazi gani na unachangia nini kwenye uchumi wa taifa,"anasisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com