Jeshi la Polisi mkoani Geita linachunguza tukio la wananchi kuchoma kituo cha Polisi Mganza pamoja na ofisi ya Chama cha Mapinduzi zilizokuwa zinapakana kwa kulituhumu Jeshi hilo kuhusika na kifo cha Enos Misalaba (32), aliyekuwa anatuhumiwa kuiba betri la gari.
Akiongea kwa njia ya simu, Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Geita Berthaneema Mlay amethibitisha tukio la wananchi kuvamia na kuchoma kituo cha Polisi ambapo mpaka sasa wanaendelea na uchunguzi kujua kiini cha tukio hilo.
“Alifikishwa kituoni pale kama baada ya masaa matatu akaanza kujisikia vibaya halafu akapelekwa hospitali kesho yake asubuhi kwenye saa 3, akawa amepoteza maisha, kwahiyo ile jamii nzima wakaamini Polisi wamehusika kwenye kifo cha kijana wao".
"Jana ilikuwa wanazika wale hawakuridhia wakasema sababu iliyotolewa kwamba ni ugonjwa sio sababu sahihi kwamba ni Polisi walimpiga wakasababisha kifo chake, kwahiyo wakachukua huo mwili wakauleta kituo cha Polisi na mwili ulikuwa ndani ya jeneza na sisi tukauchukua tukaurudisha mochwari ili tuweze kukaa na kusetle tujue ni namna gani ya kushughulikia hilo suala” ameeleza Mlay kuhusu sababu za wananchi kuvamia na kuchoma moto kituo cha Polisi
Marehemu Enos Misalaba inadaiwa alifariki kwa kupigwa na polisi kwa tuhuma za kuiba betri ya gari ambapo mke wa marehemu Regina Mathias ameelezea jinsi walivyofanya manunuzi ya betri hilo lililopelekea mme wake kupoteza Maisha.
“Akaniambia mke wangu kuna mtu anakuja ameniuzia betri umpe shilingi elfu 20, akupe hilo betrii na mimi nikamwambia haina shida, kweli akaja huyo mtu nikampa hiyo elfu 20 yeye akanipatia betri, saa 2 akaja mme wangu akafika akaoga akamaliza kuoga akaniambia naenda centre kwenye mihangaiko na mimi nikamwambia haina shida"
"Alipofika sentani akanipigia simu, mke wangu kuna mtu hilo betri namuuzia akija atakupa shilingi 50 na mimi nikamwambia haya ilipofika mida ya saa 10 mtu kweli akaja akanipatia shilingi 50, nikampatia betrii hiyo siku ikapita”, alisema Mathias.
Mke wa anaelezea mumewe alivyokuja kukamatwa na Jeshi la Polisi mpaka kufikia umauti wake.
“Wakaja watu wakasema hivi wameibiwa betri lao, hawa watu walikuja na mme wangu wakaingia mpaka ndani askari pamoja na mgambo na OCS alikuwepo wakaja na mwenye betri nae alikuwa amekuja hapo wakafika wakaingia hadi ndani hawakumuita hata mwenyekiti kuja kukagua wakaanza kukagua ndani kuvuruga kila kitu"
"Wakamaliza wakachukua ile betri niliyokuwa natumia mimi pale nyumbani wakaichukua pamoja na duramu na betri lingine lilikuwepo bovu wakachukua wakapeleka huku mme wangu wakiwa wanampiga na mimi nikasema hivi mbona mnampiga mme wangu wakasema huyu ni mwizi ametuibia, ila yule mwizi aliyeiba lile betri akalileta pale nyumbani na yeye walikuwa wamemkamata wakaja nae pale lakini hawakumshusha”, alisema Mathias.
CHANZO - EATV
Social Plugin