Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KINONDONI AKOSHWA NA KASI YA MAUNGANISHO YA MAJI MIVUMONI

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule amefurahishwa na kasi ya maunganisho ya huduma ya maji kwa Wananchi yanayoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) katika kata ua Mivumoni baada ya kukamilika kwa mradi wa usambazaji maji Makongo hadi Bagamoyo. 
Hadi sasa zaidi ya nyumba 2000 zimeshaunganishwa na huduma.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wanachi katika mkutano wa hadhara ulifanyika eneo la Mivumoni ambapo ameitaka Serikali ya Mtaa kuunda kamati ndogo ya maji itakayoshirikiana na DAWASA kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.

 Alisema kamati hiyo itakuwa daraja kati ya DAWASA na wananchi katika kushughulikia changamoto zao.

"Tunawashukuru na kuwapongeza DAWASA kwa utendaji wao wa kazi mzuri, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya wanachi wake, hivyo Serikali ya Mtaa mkawe daraja la kuwaunganisha DAWASA na wanachi hasa katika kipindi hichi ambacho maunganisho yanaendelea" amesema Mhe. Mtambule

Mhe. Mtambule ameagiza watendaji wa mitaa na wananchi kufuata utaratibu uliowekwa na DAWASA hasa suala la kulipia gharama za maunganisho mapya na kupata huduma kwa wakati bila upendeleo na amekemea vikali vitendo vya udanganyifu na rushwa vinavyofanywa na watu wasio waaminifu.

Naye, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Mivumoni Ndugu, Justin Mboka ameishukuru Serikali kwa kazi nzuri inayoendelea na ameiomba DAWASA kuendelea kufikisha huduma kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

"Tunashukuru kwa kazi ambayo inaendelea kufanywa na wenzetu wa DAWASA natoa wito kwa wananchi kuendelea kuomba huduma ya majisafi na kutunza miundombinu ya maji kwa huduma endelevu na ya uhakika" amesema Mwenyekiti Mboka

Akitoa maoni wakati wa kikao hicho Ndugu Annastazia Kalinga mkazi wa Mivumoni ameishukuru DAWASA kwa kuleta huduma ya majisafi kwani walikua wanatumia gharama kubwa kwa kununua maji kwa wasambazaji binafsi.

"Kwa kweli mmetutoa kimaso maso sisi kina mama kwa kauli mbiu yenu ya kututua ndoo kichwani inadhihirika kwetu tunashukuru sana DAWASA muwafikie wenzetu na wao wapate furaha na wao" amesema Ndugu Annastazia

Mradi wa usambazaji maji Makongo hadi Bagamoyo umetekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia. Unatarajiwa kunufaisha wananchi takribani 450,000. Mradi huo ulizinduliwa Machi 16 mwaka huu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com